Post Details

KUJITUMA USHIRIKIANO UADILIFU SIRI YA MAFANIKIO KAZINI – JAJI MSTAAFU MATUPA

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania,Devisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumu, Mhe. Sirillius Matupa amesema kujituma, kujitoa, ushirikiano, uadilifu, kuchagua na kusimamia mambo unayoyaamini ndio siri ya mafanikio katika utumishi wa umma.

 Akizungumza katika tafrija fupi ya kumuaga iliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Sheria kwa vitendo (Law School) mapema wiki hii, Jaji Mstaafu Matupa amesema kwa kufuata mambo hayo yatamuwezesha mtumishi kutekeleza majukumu yake kwa ustadi na Amani.

“Sijutii kuwa Mtumishi wa Mahakama ya Tanzania kwa kipindi chote cha utumishi wangu naondoka kifua mbele nikiiacha Taasisi yangu ikiwa imara, hivyo nawaasa watumishi kujipanga vizuri kuyapokea maisha baada ya utumishi, ni ukweli usiopingika kuna maisha baada ya utumishi wa Umma ni mazuri na hamna budi kuondoa wasiwasi changamoto ni zile zile za maisha ya kila siku”, alisema Jaji Mstaafu Matupa.

Aidha, Jaji huyo Mstaafu aliwapongeza watumishi aliofanya nao kazi kwa upendo na ushirikiano wa hali na mali katika kipindi chote alichokuwa kazini kwa ushauri, maoni, mapendekezo na hata kukosolewa pale mambo yalipokuwa yanaonekana kutokwenda sawa.

“Nashukuru kwa ushirikiano niliopata kutoka kwenu katika harakati za kuboresha utendaji wa kazi za kuwahudumia wadau wa Mahakama,” alieleza Jaji Mstaafu Matupa.

Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Devisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Lilian Mashaka alisema Jaji Matupa atakumbukwa kwa uchapa kazi wake uliotukuka, upendo, ushauri, ushirikiano na kujiamini kwake katika kutekeleza majukumu yake.

“Naamini hatutampata Jaji Matupa mwingine wa kaliba yake, alikuwa mtu wa viwango katika kazi, mnyenyekevu, msikivu na aliependa kumueshimu kila mtu aliyefanya nae kazi”, aliongeza Jaji Mashaka.  

 

Comments (0)

Leave a Comment