Post Details

MASHAURI YA MADAI YAMALIZIKE HARAKA ILI KUONGEZA KASI YA MAPAMBANO DHIDI YA UMASKINI: JAJI KIONGOZI

Published By:LYDIA CHURI

Na Lydia Churi-Mahakama

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amesema mashauri ya madai ni lazima yatazamwe kwa mapana na yakamilike kwa haraka ili wananchi watumie rasilimali na muda mwingi katika uzalishaji mali na kutoa huduma badala ya kupoteza muda mwingi kutafuta utatuzi wa mashauri hayo.

Akifungua kikao cha kitaifa cha kusukuma mashauri ya madai jijini Dar es salaam, Jaji Kiongozi alisema kuchelewa kumalizika kwa mashauri hayo kunaweza kukwamisha au kuchelewesha azma ya nchi ya kukuza uchumi na kufifisha mapambano dhidi ya umaskini.

Alisema ingawa Mahakama ndicho chombo cha mwisho katika utoaji haki, lakini  haiwezi kutekeleza jukumu hilo pasipo mchango  wa wadau wake ambao baadhi yake ni Polisi, Magereza, Takukuru, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, Mawakili na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Seikali.

Jaji Kiongozi alisema pamoja na maboresho makubwa yaliyofanyika ndani ya Mahakama endapo wadau hawatashirikishwa hayatafika mbali hivyo aliwataka wajumbe wa kamati ya kitaifa ya kusukuma mashauri kuwa daraja la kukutanisha wadau wote kutatua changamoto na kuimarisha umoja.

Akizungumzia ucheleweshwaji wa mashauri ya madai, Jaji Kiongozi alisema ucheleweshwji huo hausababishwi na mapungufu ya sheria bali ni mapungufu ya wasimamizi katika utoaji haki na wadau pamoja na maahiriho marefu na mapingamizi yasiyokuwa na sababu za msingi.

Kuhusu Tehama alisema matumizi bora ya Teknolojia hiyo ndani ya Mahakama ni nyenzo muhimu katika kuwezesha utoaji haki kwa wakati na kusogeza huduma karibu ziadi na wananchi.

“Mahakama inapoendelea kutumia Tehama katika kutoa huduma za ufunguaji, usikilizwaji na menejimenti ya mashauri, wadau katika sekta ya utoaji haki lazima tawe pamoja na kwa kasi moja”, alisisitiza.

Jaji Kiongozi alisema mwelekeo wa Mahakama kwa sasa katika matumizi ya Tehama ni kuwa Mahakama isiyotumia karatasi (Paperless Cout) na tayari imeanza na Mahakama ya wilaya ya Kigamboni kama eneo la majaribio (Pilot Court) na hivi karibuni Mahakama za wilaya zote zenye majengo mapya na ya kisasa zitafikiwa.  

Mirathi

Katika hatua nyingine, Jaji Kiongozi amesema mashauri ya mirathi huchukua muda mrefu kumalizika kutokana na ndugu na jamaa wa marehemu kushindwa kuelewana katika viako vya familia na ukoo na kuleta tofauti na uadui wao mahakamani kupitia mashauri hayo.

“Sheria na taratibu zinazoongoza mashauri ya mirathi hazina tatizo, tatizo linakuja pale ndugu na jamaa wa marehemu wanaposhindwa kuelewana kwenye vikao vyao vya familia na ukoo”, alisema Jaji Feleshi.

Alisema eneo la mirathi limegubikwa na uadui kwa ndugu na jamaa na kusababisha kutokubaliana na maamuzi ya Mahakama zilizosilkiliza shauri hivyo kuwafanya wahusika kushindana kwa kufungua mashauri ya rufaa au maombi mbalimbali kwenye Mahakama za juu.  

Alisema hali hii huchangia ucheleweshwaji kwa kuwa taratibu za mahakama hugeuzwa kuwa silaha za kukomoana na kuchelewesha kukamilika kwa mashauri ya mirathi.

Aliongeza kuwa kuchelewa kwa mashauri haya huchelewesha na hata kuwanyima warithi manufaa yao hivyo amewataka wajumbe wa kamati ya kitaifa ya kusukuma mashauri kutafuta namna bora ya kumaliza tatizo hilo.

  

      

 

Comments (0)

Leave a Comment