Post Details

MSAJILI MKUU MAHAKAMA ASISITIZA MATUMIZI YA TEHAMA MAHAKAMANI

Published By:LYDIA CHURI

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma amefanya ziara ya kikazi katika Mahakama ya Wilaya ya Momba ambapo amewasisitiza Watumishi wa Mahakama katika Wilaya hiyo kuongeza nguvu zaidi katika matumizi ya TEHAMA ili kuongeza kasi ya utendaji hatimaye haki iweze kupatikana kwa wakati.

Akizungumza na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya hiyo hivi karibuni, Mhe. Chuma alisema kuwa Mahakama imeanza utaratibu wa kutoa huduma zake bila kutumia karatasi kwa maana ya ‘paperless court’.

“Zoezi la utaratibu wa kutoa huduma bila kutumia karatasi lilianza kutekelezwa Novemba mosi , 2020 katika Mahakama ya Wilaya Kigamboniambapo TEHAMA inatumika tangu kusajili shauri hadi kuhitimishwa kwake,” alieleza Mhe. Chuma.

Msajili huyo Mkuu aliongeza kuwa jitihada za Mahakama katika kutumia TEHAMA zinaenda sambasamba na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano (5) wa Mahakama (2015-2020).

Katika ziara hiyo ya siku moja, Mhe. Chuma alipata fursa ya kumtembelea Mkuu wa Wilaya ya Momba, Bw.Juma Irando ambapo alimuomba kusaidia kutoa elimu kwa wananchi hususani kuwahimiza Wasimamizi wa mirathi kugawa na kufunga mirathi kwa wakati.

Aidha, Msajili Mkuu alimsihi Mkuu huyo wa Wilaya kuwasimamia vizuri viongozi walio chini yake hususani wanaohusika na suala ya upelelezi wa mashauri ya jinai.

Comments (0)

Leave a Comment