Post Details

WASAIDIZI WA KUMBUKUMBU WA MAHAKAMA DAR ES SALAAM WAPIGWA MSASA MFUMO MPYA WA 'e-CMS'

Published By:Mary C. Gwera

Na Eunice Lugiana, Mahakama-Dar es Salaam

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam wamefanya mafunzo kwa Wasaidizi wa Kumbukumbu kuhusu Mfumo mpya wa Kuratibu Mashauri kwa njia ya Mtandao (e-CMS). 

Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo yaliyofanyika tarehe 18 Novemba, 2023 katika ukumbi wa Mahakama Kuu Dar es Salaam,  Mtendaji wa Kanda hiyo, Bw. Moses Mashaka alisema baada ya Mfumo huo kuanza kufanya kazi alichukua hatua ya kutembelea Masjala ili kuona shughuli zinavyofanyika baada ya mfumo kuanza ndipo alipogundua kuna haja ya mafunzo ili Wasaidizi wa Kumbukumbu waweze kufanya kwa nafasi yao vizuri katika mfumo huo.

“Mtandao huo unawahusisha Majaji, Wasajili, Mahakimu na Wasaidizi wa Kumbukumbu kwa kiwango kidogo,” alisema Bw. Mashaka.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Tehama Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Bi. Elicia Meena alisema Mfumo huu unawahusisha zaidi Majaji, Wasajili na Mahakimu katika usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao ambapo Jaji au Hakimu anaingia kwenye Mfumo na kuandaa akidi moja kwa moja badala ya Msaidizi wa Kumbukumbu kuandika akidi kwenye jalada kama ilivyokuwa inafanyika mwanzo.

Alisema, katika Mfumo huo Wasaidizi wa Kumbukumbu wana nafasi ya kuwafungulia akaunti wateja wanaokuja mahakamani bila kuwa na Wakili na pia kuwapa taarifa ya mashauri hao kupitia akaunti wanazowafungulia.

Aliongeza kuwa, kwenye Mfumo huo kumeongezwa mfumo mwingine wa kutoa namba ya rejea (reference number) na pia kuangalia mashauri yaliyopangwa (cause list), mfumo huo unafahamika ‘data hub’, mfumo huu unamuwezesha Msaidizi wa Kumbukumbu kutengeneza namba ya kumbukumbu na kuangalia mashauri yaliyopangwa.

Akielezea kuhusu Mfumo huo, Afisa TEHAMA, Bw. Juma Kimaro alisema kuanzishwa kwa Mfumo huu wa kuratibu utoaji wa namba za kumbukumbu na mashauri yaliyopangwa umetengenezwa ili kuepuka kuulemea Mfumo ili kuepuka ucheleweshaji wa kusikiliza mashauri. Kimaro alisema, “Mfumo mmoja ukiratibu shughuli zote hizo unaelemewa hivyo kazi zinafanyika taratibu hata kufunguka kunakuwa taratibu sana.”

Naye, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi alifika katika mafunzo hayo kwa lengo la kuwatia  moyo washiriki wa mafunzo hayo na pia kuuliza maswali kadhaa ya ufahamu kwa ajili yake na washiriki hao.

Mafunzo hayo yamehudhuriwa pia na Maafisa Utumishi wa Mahakama Kuu na Wahasibu.

Mahakama ya Tanzania mapema mwezi huu ilianza rasmi kutumia Mfumo mpya wa Kuratibu na Kusimamia Mashauri kwa njia ya Mtandao (e-CMS Electronic Case Management System). Mfumo huu unawahusisha zaidi Majaji, Wasajili na Mahakimu.

Comments (0)

Leave a Comment