Post Details

UTATUZI MIGOGORO KWA NJIA YA USULUHISHI NCHINI LITHUANIA WAFUNGA BAADHI YA MAHAKAMA

Published By:Mary C. Gwera

Na Tiganya Vincent-Lithuania

Matumizi ya usuluhishi kwenye migogoro ikiwemo ya kifamilia imesababisha Nchi ya Lithuania kufikia hatua ya kufunga baadhi ya majengo baada ya kukosa mashauri.

Akitoa mada jana tarehe 16 Novemba, 2023 kwa ujumbe kutoka Mahakama ya Tanzania kuhusu usuluhishi katika utatuzi wa migogoro, Mshauri Mkuu wa Masuala ya Sheria na Sera kutoka Wizara ya Sheria nchini Lithuania, Bi. Reda Gabrilavic?iu?te? alisema majaribio ya matumizi ya usuluhishi yalianza mwaka 2005 na kufikia Januari, 2015 usuluhishi ulitumika katika Mahakama zote nchini humo.

Aliongeza kuwa mfumo wa upatanishi umesaidia kuleta amani ya kifamilia na kuokoa muda na pesa kwa wahusika.

Bi. Reda alisema baada ya kuanza kutumia njia ya usuluhishi katika utatuzi wa migogoro ya kifamilia imesaidia kupunguza mzigo wa mashauri kwa Majaji na hivyo kufikia kufunga baadhi ya majengo ambayo yalikuwa yakitumiwa na Mahakama katika uendeshaji wa mashauri.

Aliongeza kuwa katika Nchi hiyo Jaji anaweza kuelekeza shauri lisitumie mfumo wa kisheria na kufuata njia za usuluhishi katika kumaliza mgogoro wa pande husika.

Bi. Reda alisema Nchi hiyo ina jumla ya Wasulushi 726 ambapo kati ya hao Majaji ni 131 ambao wamesajiliwa na orodha yao imewekwa katika Tovuti.

Alisema, katika utaratibu wa Nchi hiyo Msuluhishi ni lazima awe na Elimu ya Chuo Kikuu, awe amepitia mafunzo ya usuluhishi sio chini ya saa 40 na kufaulu mitihani ya usuluhishi.

Alisema Wasuluhsi katika utekelezaji wa majukumu yao ni lazima wafuate Kanuni na Maadili stahiki.

Bi. Reda alisema kwamba, Wasuluhishi wanaokiuka  hupewa onyo na wengine huondolewa katika orodha ya Wapatanishi.

Aliongeza kwa kusema kuwa, malengo yao ya baadaye ni kutumia Wasuluhishi ambao wanatoka nje ya Jamhuri ya Lithuania na vilevile kusuluhisha katika baadhi ya mashauri ya Jinai.

 

Comments (0)

Leave a Comment