Post Details

WASAIDIZI WA KUMBUKUMBU WA MAHAKAMA KIGOMA WASISITIZWA KUTUMIA IPASAVYO MIFUMO YA TEHAMA

Published By:LYDIA CHURI

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Kigoma, Mhe. Jaji Ilvin Mugeta amefungua rasmi awamu ya pili ya mafunzo ya Wasaidizi wa Kumbukumbu juu ya mifumo ya TEHAMA huku akiwasisitiza Watumishi hao kama watendaji muhimu wa masjala kuwa wana mchango mkubwa katika kuleta tija ya utendaji kazi kupitia mifumo mbalimbali ya Mahakama.

Akifungua mafunzo hayo mwishoni mwa wiki iliyopita, Mhe. Jaji Mugeta alisema kuwa upimaji wa utendaji kazi utazingatia eneo la matumizi ya TEHAMA na kusisitiza kila mmoja kutimiza wajibu wake.

“Matumizi ya TEHAMA yamelenga kurahisisha shughuli za utoaji haki, kuongeza uwazi, ubora wa taarifa na Takwimu na kuwapunguzia gharama wadaawa” alisema Jaji Mugeta.

Mhe. Jaji Mugeta aliongeza kuwa Mahakama imewekeza katika mifumo mbalimbali inayorahisisha upatikanaji wa haki na baadhi ya mifumo hiyo ni pamoja na wa  Kusikiliza mashauri kwa njia ya Video (video conferencing), Mfumo wa kuwatambua mawakili (TAMS), Mfumo wa kusajili mashauri (JSDS II) na mfumo wa mawasiliano kwa barua pepe (Judicial mailing system).

Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Kigoma Mhe. Arnold Kirekiano alipongeza juhudi ambazo wasaidizi wa kumbukumbu wamefanya katika kuhuisha taarifa za mashauri na kusema  mafunzo hayo yatawawezesha kufanya vizuri  zaidi na kuhakikisha Kanda hiyo inakuwa ya mfano kwa usahihi wa taarifa na takwimu za mashauri.

Mafunzo hayo ya awamu ya pili katika utekelezaji wa Mpango wa ndani wa mafunzo  kwa mwaka wa fedha 2020/2021 yaliwezeshwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Kirekiano, Mtendaji wa Mahakama Kuu- Kigoma, Bw. Moses Mashaka na Afisa TEHAMA, Bw. Prosper Bonaventura Mahalala.

Comments (0)

Leave a Comment