Post Details

MAHAKAMA YA TANZANIA YAOKOA GHARAMA KATIKA UENDESHAJI WA BAADHI YA MASHAURI KWA‘VIDEO CONFERENCE'

Published By:Mary C. Gwera

Mahakama ya Rufani Tanzania, kwa mara ya kwanza,imeendesha  jumla ya mashauri nane (8) kupitia ‘video conference’ iliyofanyika kati ya Dar es Salaam na Mbeya. 

Mashauri hayo yalisikilizwa rasmi Machi 11 na Machi 12, kwa nyakati tofauti na jumla ya Majaji wanne (4) wa Mahakama hiyo ambao ni, Mhe. Jaji Rehema Mkuye, Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi, Mhe. Jaji Gerald Ndika na Mhe. Jaji Jacobs Mwambegele. 

Mashauri yote nane yalikuwa ni maombi ya kuongezewa muda ili kuwawezesha waleta maombi kufungua rufaa zao katika Mahakama ya Rufani ya Tanzania nje ya muda.Aidha, kati ya mashauri yaliyosikilizwa March 12, kupitia ‘Video Conference’ iliyopo katika Kituo cha Mafunzo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na ile iliyopo Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya, ilikuwa ni shauri la maombi ya madai kati ya   Venance Nyaringa Kazuri na  Eldard Mwesiga Sospeter lililosikilizwa na Mh Jaji Jacobs Mwambegele.

Wadaawa wote waliokuwa wakiwakilishwa na mawakili waliweza kutoa hoja zao na mwisho  Mhe. Jaji aliahidi kutoa uamuzi katika muda utakaopangwa na Wadaawa wote wa pande mbili watajulishwa.

 Katika hatua nyingine, Mhe. Jaji Mwambegele alisikiliza pia Shauri lililomhusisha Bi. Agnes Sanga dhidi ya Amon Halinga na Peter Haonga ambapo Bi. Agness Sanga ameiomba Mahakama hiyo ikubali maombi yake ya kuongezewa muda ili kusajili rufaa yake nje ya muda.

Kufuatia hatua hiyo Jaji wa Mahakama hiyo, Mhe. Jaji Mwambegele baada ya kusikiliza shauri hilo ameahidi kutoa uamuzi katika muda utakaopangwa.

Akizungumzia faida za Matumizi ya ‘video conference’, Naibu Msajili Mwandamizi, Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Elizabeth Mkwizu aliainisha faida hizo kuwa ni pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa mashauri  na kupunguza muda wa usikilizwaji wa mashauri kwa Mahakama na kwa wadau na pia ni kutekeleza kwa vitendo dira ya Mahakama ya Utoaji Haki Sawa  kwa wote na kwa wakati.

“Kwa kawaida, ili kuendesha kesi hizi, tulipaswa kuwasafirisha Wahe. Majaji, na watumishi wengine kwenda Mbeya na Sumbawanga ambapo mashauri haya yamesajiliwa ambapo ingelazimu kulipia mafuta ya magari,malazi na stahiki zingine za watumishi ,hali ambayo inatumia gharama kubwa na hurefusha muda muda  wa usikilizwaji wa mashauri,” alieleza Mhe. Mkwizu.

Mhe. Mkwizu aliongeza kuwa gharama inayotumika katika uendeshaji wa kesi kupitia ‘video conference’ ni kiasi cha shilingi 140,000/- kwa vituo vyote viwili kwa siku huku kila kituo kikitumia shilingi 70,000/-. Kwa kawaida kesi hizi zingesikilizwa kwa njia ya kawaida zingegharimu kiasi kikubwa cha fedha.

Teknolojia hii ya ‘Video conference’ imewekwa pia katika maeneo kadhaa ambayo ni Mahakama Kuu-Dar es Salaam, Mahakama Kuu- Bukoba, Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto pamoja na Gereza la Keko.

Vifaa hivi ambavyo tayari vimewekwa na vingine vitakavyowekwa katika Mahakama zitakazochaguliwa zinalenga kuwezesha uendeshaji wa mashauri na Mafunzo.

 Mahakama ya Tanzania kupitia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (5) (2015/2016-2019/2020) imelenga kuboresha huduma zake katika nyanja mbalimbali lengo likiwa ni kutoa haki sawa kwa wote na kwa wakati kama isemavyo dira yake.

Comments (0)

Leave a Comment