Post Details

UJUMBE MAHAKAMA YA TANZANIA WAKUTANA NA RAIS WA MAHAKAMA YA WILAYA VILNIUS

Published By:Mary C. Gwera

Na Tiganya Vincent,Vilnius -Lithuania

Ujumbe wa Mahakama ya Tanzania ukiongozwa na Mtendaji Mkuu, Prof. Elisante Ole Gabriel jana tarehe 15 Novemba 2023 ulikutana na Rais wa Mahakama ya Wilaya ya Mji wa Vilnius nchini Lithuania, Mhe. Viktorija Šelmien? kwa ajili ya kubadilisha uzoefu katika maeneo mbalimbali ya utoaji haki  kwa pande zote mbili.

Akizungumza mara baada ya kuwasili katika Mahakama hiyo, Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Ole Gabriel alisema ziara  hiyo imekuwa na manufaa kwa pande zote katika kufungua ukurasa wa kushirikiana katika kuboresha utoaji haki kwa wananchi wa Nchi hizo mbili.

Prof. Ole Gabriel aliwashukuru kwa mapokezi mazuri na kuwakaribisha Tanzania kwa ajili ya kuongeza ushirikiano zaidi pamoja na kubadilishana uzoefu katika kuboresha eneo la utoaji haki kwa wananchi.

Naye, Rais wa Mahakama hiyo ambaye pia ni Jaji anayejikita na kubobea katika mashauri ya Jinai (specialization in Criminal cases), Mhe. Viktorija Šelmien? alisema mfumo wa uendeshaji wa mashauri nchini humo unawagawa Majaji katika maeneo mawili ya wanaojihusisha na mashauri ya Jinai na wale wanaoshughulikia mashauri ya madai.

Alisema kwa Majaji wanaojihusisha na mashauri ya Jinai hawaruhusiwi kusikiliza na kuendesha mashauri yanayohusu madai na wale na wa madai vilevile hawapaswi kusikiliza mashauri ya Jinai.

Mhe. Viktorija alisema Nchi hiyo imekuwa na Majaji wengi wanawake ukilinganisha na wanaume, huku akibainisha kuwa, wanawake wamekuwa wakifanya vizuri katika mitihani ya kuomba kufanya kazi ya Ujaji na wamekuwa wakisifika kwa uchapaji kazi kwa bidii bila kujali maslahi makubwa.

Aliongeza wanaume wengi katika Nchi hiyo waliosomea Sheria wamekuwa wakitaka kazi ya Uwakili na nyinginezo ambazo wanalipwa maslahi makubwa.

Kadhalika, Mhe. Viktorija alisema kuwa, katika Nchi hiyo utambulisho wa mtoto katika shauri haufichi bali kuna Taasisi ambayo iko maalum kulinda haki za Watoto ambao ni waathirika.

Mhe. Viktorija alisema vifaa vilivyowekwa kama vile Kamera, kinasa sauti havionekani kwa mtoto na husaidia kwenye chumba cha pili kushuhudia maelezo ya mtoto bila hata kujua kuwa watu wanasikiliza maelezo yake.

Comments (0)

Leave a Comment