Published By: | Mary C. Gwera |
---|
Na Upendo Ngitiri- Mahakama ya Tanzania, Uswisi
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani tarehe 13 Novemba, 2023 alianza ziara yake ya kikazi kwenye Shirika la Miliki Bunifu Duniani “World Intellectual Property Organization” (WIPO) nchini Uswisi–Geneva kufuatia mualiko wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, lengo likiwa ni kujadili masuala mbalimbali ya mashirikiano baina ya Shirika hilo na Mahakama ya Tanzania.
Wakati wa hafla fupi ya ukaribisho wake pamoja na wajumbe aliombatana nao, Jaji Kiongozi alimpongeza Mkurugenzi Mkuu Daren Tang kwa kazi nzuri anayofanya kulinda na kukuza miliki bunifu duniani kote, ikiwemo nchi ya Tanzania. Alieleza kuwa kazi nzuri inayofanywa na Mkurugenzi Mkuu inaonekana kupitia programu mbalimbali zinazosimamiwa na WIPO.
Jaji Kiongozi aliwashukuru WIPO kwa mchango mkubwa ulioboresha utoaji haki kwenye eneo la miliki bunifu nchini Tanzania.
Mhe. Siyani alieleza kuwa, Mahakama ya Tanzania imenufaika na ushirikiano huo kupitia mikutano, makongamono na mafunzo mbalimbali, miongozo ya kufundishia iliyoandaliwa mahsusi kwa Mahakama ya Tanzania, uchapishaji wa maamuzi ya Mahakama ya Tanzania na muhtasari wa maamuzi hayo kwenye kanzidata ya kielektroniki, maarufu kama WIPO Lex Database.
Aliwashukuru pia WIPO kwa kushirikina na Mahakama ya Tanzania katika kuboresha usuluhishi wa migogoro kupitia utoaji wa mafunzo juu ya usuluhishi na huduma za usuluhishi kwa njia ya mtandao. Jaji Kiongozi alitumia pia fursa hiyo kushukuru WIPO kwa kuwateua Majaji saba wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuwa miongoni mwa wasuluhishi wa WIPO.
Jaji Kiongozi alieleza pia kuwa jumla ya Maafisa wa Mahakama (Majaji na Mahakimu) 815 wameshanufaika na mafunzo pamoja na shughuli mbalimbali zinazoratibiwa na WIPO kwa kushirikina na Mahakama ya Tanzania. Alimshukuru Mkurugenzi wa WIPO Judicial Institute, Bi. Eu-Njoo –Min WIPO na Maafisa Waandamizi wengine kutoka WIPO Arbitration and Mediation Centre, WIPO Academy, WIPO Division for Africa na WIPO Division for LDCs kwa kufanya kazi kwa karibu na Mahakama ya Tanzania.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dkt. Aleman Marco, alimshukuru Jaji kiongozi na wajumbe aliombatana nao kwa kutembelea shirika hilo. Dkt. Aleman alieleza kuwa WIPO wanashukuru na kuthamini ushirikiano wa karibu baina ya Mahakama ya Tanzania na WIPO na akaahidi kuendelea kushirikina na Mahakama ya Tanzania kwa karibu zaidi.
Kufuatia majadiliano yaliyofanyika, Dkt. Aleman alieleza kuwa Shirika hilo kwa kushirikina na Mahakama litaandaa mafunzo ya ana kwa ana mwaka kesho nchini Tanzania yatakayoendeshwa na Majaji wabobezi kwenye eneo hili kutoka nchi mbalimbali Duniani na Wataalamu kutoka WIPO.
Alieleza pia kuwa WIPO watahuisha maamuzi ya Mahakama ya Tanzania kwa kuchapisha maamuzi yaliyotolewa na Mahakama ya Tanzania katika miaka ya karibu sambamba na kushirikina na Mahakama ya Tanzania kuanda muhtasari wa Maamuzi hayo.
Mbali na hilo, alieleza kuwa wataalumu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wataangalia namna ya kuunganisha (intergration) WIPO Lex judgment database na tovuti ya Mahakama ili Majaji na Mahakimu waweze kupata maamuzi yaliyopo kwenye WIPO lex moja kwa moja kupitia tovuti ya Mahakama.
Aliongeza kuwa wataangalia namana bora ya kushirikisha maafisa wa Mahakama kutoka Zanzibar katika shughuli mbalimbali zinazofanywa na WIPO kwa madhumuni ya kuboresha utoaji haki.
Jaji Kiongozi alipata pia fursa ya kupitishwa kwenye kazi mbalimbali zinazofanywa na WIPO Academy na kuahidiwa kuwa Kituo hicho kitaanda kozi mahsusi kwa maana ya customized IP course kwa ajili ya Majaji na Mahakimu wa Tanzania.
Wajumbe waliongozana na Jaji Kiongozi katika ziara hiyo ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Wilbert Chuma, Naibu Msajili na Katibu wa Jaji Kiongozi, Mhe.Aidan Mwilapa, Hakimu Mkazi Mkuu na Katibu wa Msajili Mkuu, Mhe. Jovine Bishanga, Hakimu Mkazi Mwandamizi na Afisa Kiungo baina ya Mahakama ya Tanzania na WIPO, Mhe. Upendo Ngitiri.