Post Details

TUMIENI MAJUKWAA YENU KUELIMISHA WANANCHI MABORESHO YA MAHAKAMA: MSAJILI MKUU

Published By:LYDIA CHURI

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Martine Chuma amewaomba Wakuu wa Wilaya nchini kote kutumia majukwaa yao kuwaelimisha wananchi juu ya Maboresho na mageuzi makubwa ya kiutendaji yanayofanywa na Mahakama ya Tanzania ili kuongeza ustawi katika utoaji wa haki kwa wakati na kwa wote. 

Akiongea na Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Bw. Godfrey Mheluka wakati alipomtembelea Ofisini kwake alipokuwa kwenye ziara ya kikazi kukagua utendaji wa shughuli za Mahakama hivi karibuni, Mhe. Chuma alisema, Mahakama ya Tanzania imefanya maboresho makubwa katika nyanja mbalimbali ili kuboresha huduma ya utoaji haki kwa wananchi wake kupitia mpango mkakati wake wa miaka mitano ulioanza mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021.

Mhe. Chuma alisema, maeneo ambayo yamefanyiwa mageuzi makubwa ni ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya majengo na kukarabati mengine, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika usikilizaji wa mashauri kwa njia ya Mahakama Mtandao, utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka, kuanzishwa kwa Mahakama isiyotumia karatasi maarufu kama “Paperless Court”, na Mahakama inayotembea maarufu kama “Mobile Court”.

Maeneo mengine aliyoyaeleza Mhe. Chuma ni kusajili mashauri kwa njia ya mtandao maarufu kama “E – Filing”, kusajili mashauri yanapokelewa Mahakamani na kuyahuisha kwenye mfumo maalumu ujulikanao kama “JSDS II”, kutambua Mawakili waliohai na wasio huisha leseni zao na mfumo wa kuhifadhi maamuzi, hukumu za mashauri, kanuni na sheria mbalimbali mfumo huu unajulikana kama “TANZLII”.

Ada na tozo za huduma za Mahakama kwa kutumia mfumo wa kielektroniki hii imepunguza kwa kiasi kikubwa mianya ya rushwa katika utoaji wa huduma, utambuzi wa hali za majengo ya Mahakama nchi nzima kupitia mfumo wa mtandao maarufu kama “Judical Maping System” na kusimamia kwa karibu nidhamu za watumishi.

“Ni muhimu sana watu waijue Mahakama ni nini na inafanya nini, hali kadhalika Mahakama yenyewe inapaswa kuwajua watu wake inaowahudumia, ninatoa rai kwenu kuisaidia Mahakama kutoa elimu ili wananchi waelewe kuwa Taasisi yao ipo kwa lengo la kuwasaidia katika utatuzi wa migogoro kwa weledi mkubwa”, alisema Mhe. Chuma.

Msajili Mkuu aliwaomba pia Wakuu wa Wilaya kupitia majukwaa yao kulipa kipaumbele suala la mirathi, kutoa elimu kwa wananchi kwa kushirikiana na Mahakama zilizopo kwenye maeneo yao, licha ya kuwa Mahakama imekuwa ikitoa elimu kwa wadau wake lakini haiwezi kuwafikia wananchi wote kwa wakati mmoja.

“Uzoefu unaonyesha kuwa wadaawa wengi wanaofungua mirathi mahakamani na kukamilisha taratibu za kuteuliwa kuwa wasimamizi hawatimizi wajibu wao kisheria kwa kurudi mahakamani kufunga mirathi yao licha ya kuelezwa na Mahakama kuwa ni takwa la kisheria kufanya hivyo, shauri la mirathi haliishii pale tu mtu anapoteuliwa, linakamilika pale msimamizi anapoleta mahakamani taarifa ya kukamilika utekelezaji wa shughuli zote za kugawa mali za marehemu kwa usahihi kwa wanufaika wa mirathi hiyo,” alifafanua Msajili Mkuu.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Bw. Godfrey Mheluka amehihakikishia Mahakama ya Tanzania kuendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali kuhakikisha Mahakama inafikia malengo yake iliyojipangia, kwa sasa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya inamahusiano ya karibu na Mahakama katika masuala ya kiutendaji hali ni shwari kabisa.

“Kupitia Ofisi yangu na Kamati yangu ya usalama nimefarijika kuona Mahakama imepiga hatua kubwa katika mambo mengi makubwa hasa kuimarisha huduma za utoaji haki nchini kwa kuanzisha na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika shughuli zake,” alisema Bw. Mheluka.

Katika upande mwingine Mhe. Chuma aliwakubusha watumishi wa Wilaya hiyo juu ya umuhimu wa mahusiano kazini na kupeana taarifa sahihi za kiutendaji ili kuondoa migongano isiyo ya lazima, aliyasema hayo alipokuwa akipokea taarifa ya utendaji kazi ya Mahakama ya Wilaya ya Karagwe na kyerwa.

Mhe. Chuma aliwataka Watumishi kutunza maadili ya kazi zao bila kuathiri shughuli zingine za kijamii, ikiwa ni pamoja na kutoa huduma kwa wateja bila kubagua, kutumia lugha za staha na kuwa wakali pale wanaposhindwa kutatua kero za wateja kwa kuomba msaada kwa kiongozi wa ngazi ya juu, itaonyesha mshikamano wakati wa kutimiza majukumu yenu.

“Kila mtumishi anatambua wajibu wake awapo kazini tutimize wajibu wetu na kuongeza bidii ya kazi ili tuweze kufikia malengo ya kila mmoja wetu na ya Taasisi kwa ujumla, hii itaondoa dhana ya kusukumwa na viongozi wetu tuwapo kazini” alisisitiza Mhe. Chuma.

Kwa upande wa mashauri amewataka Mahakimu kuzingatia taratibu za kisheria na kikanuni pale wanaposikiliza mashauri ya jinai matharani kuweka kumbukumbu sahihi wakati wa utoaji wa dhamana kwa washitakiwa, kumbukumbu zinatakiwa kujieleza zenyewe badala ya kutegemea nyaraka za utambulisho au barua ya mdhamini, alisema Mhe. Chuma

“Toeni sababu za msingi zenye mashiko pale mnaposikiliza mashauri ya mirathi nje ya utaratibu wa kisheria ili ukaguzi utakapo fanyika muwe kwenye upande salama usiotiliwa shaka na viongozi wako”, alisistiza Msajili Mkuu.

 

Comments (0)

Leave a Comment