Published By: | innocent.kansha |
---|
Na. Stephen Kapiga – Mahakama, Mwanza.
Wananchi na Wadau wa Mahakama mkoani Mwanza wamesisitizwa juu ya umuhimu wa kutumia Kituo cha Huduma kwa Mteja (call center) cha Mahakama ya Tanzania kutoa maoni, malalamiko pale ambapo wataona hawajaridhika na huduma waliyopatiwa kuliko kukaa na dukuduku moyoni au kuwaambia watu ambao hawataweza kuwapatia ufumbuzi wowote.
Akizungumza na wadau na wateja wa Mahakama katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kilichopo jijini Mwanza hivi karibuni Hakimu Mkazi Mwandamizi Mhe. Denice Mlashani ambaye pia ni mchakata taarifa za wateja katika kituo hicho, amesema kuwa kituo hicho kilianzishwa na Mahakama ya Tanzania mnamo tarehe 01 Machi, 2022 kikiwa na lengo la kupokea mrejesho kutoka kwa wateja wa Mahakama juu ya namna huduma zinazotolewa na Mahakama kama zinakidhi viwango na matamanio ya wadau ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama wa awamu ya pili wa mwaka 2020/21 – 2024/25 ukiainishwa na nguzo ya tatu ya ushirikishwaji wa wadau na kujenga imani kwa wananchi.
“kuanzishwa kwa kituo hiki kumekuwa na faida kubwa sana kwa wananchi ambao ndiyo wadau wakubwa wa Mahakama kwani imewawezesha kutoa dukuduku zao juu ya huduma za kimahakama na Mahakama pia inapata wasaa wa kujitathimini juu ya ubora wa huduma inayoitoa kwa wananchi na hivyo kuiwezesha Mahakama kufanya maboresho kwenye maeneo inayoyalalamikiwa zaidi na wananchi mfano eneo la mirathi,utekelezaji wa uamuzi na dhamana” alisema Mhe. Mlashani
Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mhe. Yasitha Kingwila alisema, tangu kuanzishwa kwa kituo hicho,jumla ya taarifa 2,751 ikiwa ni maoni, mapendekezo,malalamiko au maulizo yamepokelewa na kituo hicho, na kati ya hiyo, taarifa 2,740 zimefanyiwa kazi na wateja kupatiwa mrejesho ambao ni sawa na asilimia 98.6 huku taarifa 11 zikisubili ufuatiliaji.
“Lalamiko ni siri, lazima lalamiko lichakatwe kwa usiri mkubwa hata afisa anayelalamikiwa asijue kuwa kuna lalamiko dhidi yake, hii inalenga kuongeza imani kwa mtu aliyeotoa taarifa, na lalamiko lazima lishughulikiwe ndani ya siku saba (7) liwe limepatiwa majibu na hii ni kwa mujibu wa mkataba wa huduma kwa mteja na lalamiko linapozidi siku hizo saba (7) halijapitiwa majibu ama ufumbuzi basi ni lazima liwasilishwe kwa msimamizi ambaye ataliwasilisha sehemu husika” alisema Mhe. Kingwila.
Aidha, Mhe. Kingwila aliongeza kuwa katika kituo hicho wanatumia njia mbalimbali za upokeaji wa mrejesho kutoka kwa wateja kwa kutumia simu ya mkononi kwa kupiga simu au kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa kutumia namba ya simu 0752500400 na 0739502 401ambazo huwa hewani kwa masaa yote 24 kwa siku ndani ya siku zote saba (7) za wiki.Pia mrejesho unaweza kutumwa kupitia barua pepe ya maoni@judiciary.go.tz na ccamirathi@judiciary.go.tz au kupitia tovuti ya ya Mahakama ya www.judiciary,go.tz chini ya sanduku la kutoa maoni ya huduma za Mahakama.