Post Details

MSAJILI WA MAHAKAMA YA KIMBARI AAHIDI USHIRIKIANO

Published By:LYDIA CHURI

Msajili wa Mahakama ya Kimataifa ya Kesi Masalia za Mauaji ya Kimbari ‘IRMCT’, Bw. Abubacarr Tambadou ameahidi kuendeleza ushirikiano wa utendaji kazi baina ya Mahakama hiyo na Mahakama ya Tanzania.

Akizungumza wakati alimpotembelea Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ofisini kwake leo Desemba 02, 2020, Msajili huyo alisema kuwa yupo tayari kuendeleza kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na ‘IRMCT’ kwa maslahi ya Taifa.

 “Nina furaha kukubali ombi langu la kuonana na wewe licha ya kuwa na majukumu mengi ya kazi, lengo la mimi kuja kukutembelea ni kujitambulisha rasmi na kuomba kuendeleza ushirikiano wa kikazi baina yetu,” alieleza Bw. Tambadou.

Vilevile, Bw. Tambadou alieleza kuwa Mahakama ya Tanzania itumie vyema uwepo wa Mahakama ya Kimataifa ya Kesi Masalia za Mauaji ya Kimbari ‘IRMCT’ kama tija ya kujua zaidi sheria za kimataifa.

Naye, Mhe. Jaji Mkuu alimuahidi Msajili huyo kutoa ushirikiano zaidi na kuahidi kumtembelea pindi atakapokuwa Arusha.

Aidha; Mhe. Jaji Mkuu alipataa wasaa wa kumueleza Msajili huyo kuwa Mahakama ipo katika maboresho mbalimbali yanayolenga kurahisisha na kusogeza huduma za haki karibu zaidi na wananchi.

Hali kadhalika Mhe. Jaji Prof. Juma alimueleza Bw. Tambadou kuwa Mahakama ya Tanzania kwa sasa ipo katika maandalizi ya kuadhimisha miaka 100 ya kuanzishwa kwa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Bw. Abubacarr Tambadou alichaguliwa kuwa Msajili wa Mahakama hiyo Julai mosi mwaka huu.

Comments (0)

Leave a Comment