Post Details

TUBORESHE MASLAHI YA WATUMISHI KUONGEZA NGUVU KAZI; MSAJILI MKUU

Published By:LYDIA CHURI

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma amewaagiza Watendaji wa Mahakama kuwapa motisha watumishi wa Mhimili huo hasa wale wanaohudumu nafasi zaidi ya moja ili kuongeza tija kazini.

Akizungumza Novemba 27, 2020 katika mkutano na watumishi wa Mahakama Kanda ya Bukoba uliofanyika katika Ukumbi wa Mahakama Kuu ya Kanda hiyo, Mhe. Chuma alisema tatizo la upungufu wa watumishi lipo kwa nchi nzima na linashughulikiwa kwa kadiri vibali vya ajira vinapotolewa.

 “Unakuta kwenye kituo kuna Mtumishi kaajiriwa kada yake ni Mlinzi lakini anafanya kazi ya mtunza kumbukumbu, anashughulikia mfumo wa kusajili na kuhuisha mashauri (JSDS II) na wakati huo huo yeye anatumika kama dereva kwenye kituo chake cha kazi, sasa mtumishi kama huyu anatakiwa apewe motisha ya kazi”, alisema Msajili Mkuu.

Mhe. Chuma alisema, shughuli za Mahakama haziwezi kusimama kutokana na upungufu wa watumishi hivyo hakuna budi kutumia vyema rasilimali watu iliyopo pamoja na kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi, kuwajali watumishi wenye uwezo wa kufanya jukumu zaidi ya moja kwa kuwapa motisha ili kazi za Taasisi zisonge mbele.

Kwa upande mwingine, Msajili Mkuu amewaagiza Maafisa Utumishi na Tawala kutenga muda wa kutoa elimu kwa Watumishi kuhusu masuala yanayowatatiza ili kuondoa sintofahamu na kupata taarifa sahihi, mfano: mambo yanayohusu michango kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, mapunjo na nyongeza za mishahara, upandishwaji wa vyeo (madaraja) ikiwemo miongozo na miundo ya kiutumishi kuwongezea uelewa zaidi watumishi.

Kwa upande wa mashauri, Msajili Mkuu amewakumbusha Mahakimu kuzingatia waraka alioutoa wa kumaliza mashauri mlundikano ifikapo Desemba 2020 kwa yale mashauri walio na mamlaka nayo.

Mhe. Chuma aliwasisitiza pia watumishi hao kuzingatia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kutumia mifumo ya TEHAMA iliyopo Mahakama kama Mfumo wa kuratibu na kusajili Mashauri (JSDS2), matumizi ya vioski vya kusajilia kesi kwa njia ya mtandao “E – Filing” na mingineyo.

 

Comments (0)

Leave a Comment