Post Details

JAJI KAHYOZA AWATAKA MAHAKIMU KUJIBIDISHA KUSOMA SHERIA NA KUZITAFSIRI KWA UMAKINI

Published By:LYDIA CHURI

Na Francisca Swai- Mahakama Kuu Musoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. John Rugalema Kahyoza amewataka Mahakimu wote walioko katika Kanda ya Musoma kutumia taaluma yao kujibidisha kusoma sheria na kuzitafsiri kwa umakini.

Akifungua mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri katika Mahakama za Mwanzo kwa Mahakimu 36 wa Kanda hiyo, Mhe. Jaji Kahyoza alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kutatua changamoto zilizojitokeza wakati alipofanya ukaguzi wa robo ya tatu ya mwaka 2020 katika baadhi ya Mahakama za Mwanzo zilizopo kwenye kanda ya Musoma.

Aidha, Mafunzo hayo yalijikita katika taratibu za uendeshaji wa mashauri ya mirathi, mashauri ya madai, mashauri ya jinai, uandishi wa hukumu kwa Mahakama za Mwanzo na za Wilaya pamoja na utekelezaji wa hukumu.

Katika mashauri ya mirathi, Mhe. Jaji Kahyoza kwa kushirikiana na Mkaguzi wa Ndani wa Mahakama Kuu kanda ya Musoma Bw. Andala Odock, waliwasisitiza Mahakimu hao kuzingatia taratibu zote za msingi tangu kupokelewa kwa shauri la mirathi hadi kufungwa, zikiwepo taratibu za kuthibitisha msimamizi wa mirathi, namna ya kutunza wosia, kuzingatia mgawanyo wa mali kwa warithi, mchakato wa malipo, na kufunga mirathi.

Jaji Kahyoza aliwasisitiza Mahakimu hao umuhimu wa kufungua mashauri ya mirathi pale taratibu zote zinapokamilika pia mashauri hayo yafunguliwe eneo analotoka marehemu kuepusha ufunguaji wa shauri moja mara mbili.

Kwa upande wa mashauri ya madai na jinai, Mhe, Kahyoza, aliwataka Mahakimu hao kuzingatia sheria na kuwa makini katika kurekodi ushahidi unaotolewa mahakamani na hatua zote muhimu hadi kufikia wakati wa kutoa hukumu. Pia aliwakumbusha taratibu za ukamataji mali wakati wa kukaza hukumu.

Naye Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Musoma, Mhe.  Zephrine Galeba, alimpongeza Jaji Mfawidhi kwa kuandaa mafunzo hayo elekezi ya kujengeana uwezo na kukubali yafanyike kila robo mwaka kwani yatasaidia sana kuboresha utendaji kazi hasa kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo ambao huko ndiko mashauri mengi yanaanzia.

Jaji Galeba pia aliwataka washiriki wote kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili ya kazi pamoja na sheria ili kutoa maamuzi kwa uhuru jambo ambalo litalinda uhuru wa Mahakama.

Comments (0)

Leave a Comment