Post Details

CHUO CHA MAHAKAMA LUSHOTO CHAANDAA ‘BONANZA’

Published By:Mary C. Gwera

Chuo cha Uongozi wa Mahakama ‘IJA’ Lushoto kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali zimeshiriki katika bonanza la michezo la ‘IJA Bonanza 2020’ lengo likiwa ni kusherehekea miaka 20 toka kuanzishwa kwa chuo hicho.

 

Bonanza hilo lililoandaliwa na chuo lilifanyika hivi karibuni katika viwanja vya Chuo hicho huku likishirikisha takribani vilabu 30 vya mwendo pole “jogging” kutoka katika taasisi za Serikali, vyombo vya Habari, Mashirika ya Umma, mashirika binafsi, vilabu vya michezo, wanafunzi wa shule za Sekondari na Msingi za Wilayani Lushoto.

 

Akizungumza na washiriki wa Bonanza hilo, Mgeni rasmi ambaye alikuwa Mkuu wa Chuo hicho, Mhe. Jaji. Dkt. Paul Kihwelo Jaji wa Mahakama kuu ya Tanzania alisema kuwa lengo kuu la Bonanaza hilo ni kusherehekea miaka 20 toka kuanzishwa kwa Chuo hicho na kueleza kuwa bonanza hilo lililoitwa ‘IJA Bonanza 2020’ limebeba vitu vingi ambavyo ni kudumisha mahusisano mema katika kujenga ushirikiano  na mshikamano kati ya Chuo na jamii kwa ujumla.

 

“Bonanza hili pia linalenga kuwahamasisha Watumishi wa chuo umuhimu wa mazoezi katika kujenga afya njema ili kuepuka magonjwa yasiyoambukizwa,” aliongeza Mkuu huyo wa Chuo.

Michezo iliyofanyika ilikuwa ni mbio za mwendo pole za kuzunguka viunga vya Wilayani Lushoto kwa takribani kilometa nane (8), mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa wavu, kukimbiza kuku, kukuna nazi, kuvuta kamba, kuruka kamba, kukimbia na magunia, kukimbia na ndimu na mashindano ya kula.

Bonanza hili ni mwendelezo wa matukio mbalimbali yaliyofanywa na Chuo katika  kuelekea kilele cha miaka ishirini ya Chuo toka kuanzishwa kwake ambapo tarehe 2 Novemba, Watumishi wa Chuo walifanya usafi katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto na siku iliyofuata Watumishi hao walikwenda katika  kituo cha kulelea Watoto yatima Irente ambapo walitoa msaada wa vitu mbalimbali. 

Comments (0)

Leave a Comment