Post Details

TUSHIRIKIANE KUBORESHA HUDUMA YA UTOAJI HAKI; JAJI KIONGOZI

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ametoa rai kwa wananchi kuiunga mkono Mahakama katika jitihada za  kuhakikisha kuwa Mhimili huo unatekeleza jukumu lake la msingi la uondoshaji wa mashauri kwa wakati.

Akizungumza mara baada ya hafla ya kuwaaga kitaaluma Majaji wastaafu tisa (9) wa Mahakama Kuu ya Tanzania iliyofanyika Novemba 13, 2020 katika Ukumbi wa Mahakama Kuu Dar es Salaam, Mhe. Jaji Kiongozi alisema kuwa Mahakama imejipanga thabiti hivyo inahitaji ushirikiano ili kufikia malengo iliyojiwekea.

“Kuna changamoto kubwa sana ya wananchi kuchelewesha kesi, aidha kwa kuchelewesha kutoa Ushahidi, kutelekeza kesi na mengineyo hali ambayo inakwamisha mashauri kukamilika kwa wakati,” alisema Mhe. Jaji Dkt. Feleshi.

Aidha, Mhe. Jaji Kiongozi aliwataka pia wananchi kutumia mifumo ya Mahakama iliyopo ikiwemo Mfumo wa Kuratibu na Kusajili Mashauri kwa njia ya Kiilektroniki (JSDS) na mingineyo ili kuwawezesha kupata haki zao.

“Mahakama ya Tanzania imejipanga vilivyo kuendelea na maboresho mbalimbali yote yakiwa yanalenga kuboresha huduma ya utoaji haki kwa wananchi ili kuweza kukua kiuchumi na kuwa na ustawi kwa taifa.

Katika mahoajiano yake na Waandishi wa Habari, Mhe. Jaji Kiongozi alizungumzia pia maandalizi ya Mahakama Kuu ya Tanzania ya kuelekea kusherehekea maadhimisho ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1921.

Naye Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, Mhe. Dkt. Fauz Twaib, miongoni mwa Majaji walioagwa kitaaluma alitoa rai kwa Majaji na Watumishi wa Mahakama waliobaki kuendelea kuwatumikia vyema wananchi huku akieleza kutosahau jinsi alivyosimamia na kuendesha kesi ya Kikatiba kati ya Saed Kubenea dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kwa upande wake, Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Hamis Kalombola ameeleza kuwa kabla ya kustaafu alipendelea kufanya usuluhishi katika masuala ya kifamilia.

“Mimi napenda familia, hivyo miongoni mwa mashauri niliyokuwa napenda kusikiliza ni mashauri ya Watoto na familia kwa ujumla, nilikuwa napenda kufanya usuluhishi ili maridhiano yaweze kufikiwa baina ya pande zote mbili bila kinyongo,” alisema Jaji Mstaafu Kalombola.

Miongoni mwa Waheshimiwa Majaji wastaafu walioagwa leo ni pamoja na marehemu Jaji Upendo Msuya ambapo Mhe. Jaji Kiongozi amesema kuwa Mahakama inathamini na kujali mchango wake kwa Mhimili huo wakati wa utumishi wake.

Majaji Wastaafu wengine walioagwa ni pamoja na Mhe. Sekieti Kihiyo, Mhe. Hamisa Kalombola, Mhe. Pellagia Khaday, Mhe. Awadhi Bawazir, Mhe. Sirilius Matupa, Julius Mallaba, Mhe. Dkt. Fauz Twaib na Mhe. Sophia Wambura.

 

Comments (0)

Leave a Comment