Post Details

JAJI MKUU WA TANZANIA AMUAPISHA RAIS DKT JOHN MAGUFULI

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemuapisha rasmi Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliyeshinda kiti cha Urais baada ya kutangazwa mshindi kufuatia kukamilika kwa uchaguzi mkuu wa Taifa uliofanyika Oktoba 28, 2020.

Sambasamba na hilo katika hafla hiyo ya Uapisho wa Mhe. Rais wa awamu ya tano (5) anayetumikia nafasi hiyo kwa awamu ya pili, Mhe. Jaji Mkuu alimuapisha pia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma mapema Novemba 05, mwaka huu.

Akizungumza na wananchi mara baada ya kuapishwa rasmi, Rais Magufuli aliwashukuru Watanzania kwa kumpatia kura nyingi za ushindi na kuwaahidi kushirikiana nao katika kuleta maendeleo ya Taifa.

“Uchaguzi umekwisha, sasa tuchape kazi, napenda kuwahakikishia kama ilivyokuwa kwenye miaka mitano iliyopita na kwa miaka mitano ijayo nitaendeleza na kutimiza yale yote niliyoahidi,” alisema Rais Dkt. Magufuli.

Mhe. Rais aliongeza kuwa ataendelea kuimarisha ulinzi wa rasilimali zilizopo nchini ili ziendelee kutoa ajira, kuongeza fursa za uwekezaji na kutatua kero mbalimbali.

Katika hatua nyingine Mhe. Rais amesema Serikali itaendelea na mapambano dhidi ya rushwa na ubadhilifu wa mali za umma, kukamilisha miradi mikubwa iliyoanza na kutekeleza mingine mipya.

Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Museveni aliyehudhuria katika hafla hiyo amempongeza Mhe. Rais kwa ushindi aliopata na kuwapongeza Watanzania kwa uchaguzi wa amani na wa kidemokrasia na kuwataka kuendeleza uzalendo aliouacha Baba wa Taifa, Hayatti Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Hafla hiyo muhimu kwa Taifa ilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali.

Comments (0)

Leave a Comment