Post Details

SHIRIKIANENI KWA MASLAHI YA TAASISI – JAJI MSTAAFU WAMBURA

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Mfawidhi Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Sophia Wambura amewataka watumishi wa Mahakama ya Tanzania kufanya kazi kwa upendo, ushirikiano na uadilifu ili kuleta tija kwa Taasisi.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kumuaga baada ya kustaafu rasmi iliyofanyika katika Mahakama hiyo Oktoba 23 mwaka huu, Mhe. Jaji Mstaafu Wambura alisema kufanya kazi kama kama timu kutawezesha malengo yao na ya Taasisi kutimia.

“Ili mkono ukamilike ni lazima kila kidole kiwepo, ndipo mkono unaweza kufanya kazi kwa ukamilifu na ufanisi ndivyo basi tunatakiwa kama watumishi kufanya kazi kwa ushirikiano na kufikia mafanikio kwa maslahi mapana zaidi”, alisema Jaji .

Jaji Wambura aliongeza kwa kuzungumzia nafasi ya kiongozi katika kufanikisha hilo huku akisema kuwa. “Kiongozi bora ni mtu anayetumia muda wake kuonyesha dira ya kuwafikisha Watu kwenye hatima ya mafanikio ya mtu moja moja na hata Taasisi anayoiongoza kwa kusimamia uwazi, uwajibikaji na mahusiano mazuri pahala pa kazi.”

Aidha, Mhe. Jaji Mstaafu Wambura aliwaeleza watumishi hao kuwa katika kutimiza majukumu yao ni lazima waige kundi la ndege warukao angani bila kuongozwa na mtu bali hutumia karama walionayo na kufikia hatima yao kwa juhudi na ushirikiano wao. “Kila Mtumishi aliyepo hapa yupo kwa sababu na si bure hivyo anatakiwa kuonyesha karama ulizonazo kwa kushirikiana na wengine ili malengo yenu kama Watumishi na Taasisi yenu yatimie.”

Jaji Wambura aliwakumbusha watumishi kuzingatia maadili ya kazi ili kutoharibu taswira ya Taasisi na kupoteza imani ya Umma unaouhudumia, Viongozi wanapaswa kutoa maelekezo ya mara kwa mara kuwakumbusha watumishi masuala muhimu ya kinidhamu.

Kwa upande mwingine, Mhe. Jaji Wambura aliwataka Watumishi kutoridhika na nafasi zao kazini aliwaasa kutafuta njia mbalimbali za kuongeza na kujiendeleza kielimu ili kutafuta fursa zaidi na kupanua wigo wa ujuzi na umahiri ili kutimiza majuku yao kwa ufasaha na weledi mkubwa zaidi.

Awali akitoa neno la utangulizi kwa niaba ya watumishi, Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Devisheni ya Kazi, Mhe. Imani Daud Aboud alisema kuwa wangependa kuendelea kuwa na Jaji Mstaafu Wambura kwa ari ya utendaji kazi wake ila kwa mujibu wa sheria hana budi kupumzika katika utumishi.

Mhe. Jaji Aboud aliongeza kuwa Jaji Mstaafu Wambura ni mtu aliyekuwa na upendo wa hali ya juu kazini, ushirikiano, kusimamia nidhamu za watumishi, alikuwa mtiifu na mwadilifu, aliongeza kuwa alikuwa mpenda haki asiye na makuu na lionyesha unyenyekevu siku zote na kiongozi hodari.

Naye, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Zainab Muruke alimuelezea Jaji Mstaafu Sophia Wambura kama mfanyakazi hodari mwenye msimamo imara wa kusimamia mambo anayoyaamini katika kazi, kuwatia hari watumishi hasa wa jinsia ya kike na kuwaasa watumishi kutobweteka kujiendeleza kitaaluma ili kuboresha ufanisi kazini

Jaji Mstaafu Sophia Wambura amestaafu baada ya kuhutumikia Muhimili wa Mahakama kwa takribani miaka 35 katika nyadhifa mbalimbali.

Comments (0)

Leave a Comment