Post Details

WANANCHI WA SENGEREMA KUSOGEZEWA HUDUMA ZA UPATIKANAJI HAKI

Published By:LYDIA CHURI

Na Lydia Churi- Mahakama Mwanza.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ameiomba Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza kusaidia upatikanaji wa gereza lingine katika wilaya hiyo ili kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.

Akizungumza na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Emmanuel Kipole pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama, Jaji Kiongozi amesema bila ya kuwa na mkakati madhubuti wa kuhakikisha kunakuwa na gereza lingine Sengerema, ni wazi mashauri hayatamalizika kwa wakati mahakamani.

Alisema katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu, Mahakama ya wilaya ya Sengerema ilisajili mashauri 329 na kati ya hayo, mashauri 325 yaliamuliwa na yaliyobaki yaklikuwa ni 118. Aliongeza kuwa sababu kubwa ya mashauri kubaki ni kukosekana kwa magereza kwenye wilaya hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya hiyo iliyosomwa kwa Jaji Kiongozi, mahabusu hufikishwa mahakamani mara mbili kwa wiki kwa ajili ya kusikilizwa kwa mashauri yao hali inayosababisha mashauri kutokumalizika kwa wakati.

Akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita pamoja na Mahakama ya wilaya ya Sengerema kwa nyakati tofauti, Dkt. Feleshi aliwataka watumishi hao kujiepusha na vitendo vya rushwa na ukosefu wa maadili, kuacha  kuchongeana pasipokuwa na sababu za msingi na kuchafuana, badala yake wathaminiane na kuheshimiana kila moja katika kada yake.

Aliwataka watumishi hao kujiendeleza kielimu kwenye kada nje ya kada walizoajiriwa ili kuongeza ujuzi wa masuala mbalimbali. “Tujitahidi kujenga uwezo na thamani yetu, tusifanye kazi kwa mazoea” alisema. 

Naye Mkuu wa wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole alielezea changamoto inayotokana na ukubwa wa wilaya yake kwamba wananchi wengine wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata huduma za Mahakama makao makuu ya wilaya hiyo.

Alisema wilaya ya Sengerema inazo Tarafa 2 na kata 47 ambapo kata 5 kati ya hizo zipo maeneo ya visiwani umbali wa zaidi ya kilometa 100 kutoka makao makuu ya wilaya hiyo hivyo wananchi wengine hutumia gharama kubwa kufuata haki zao.

Aidha Mkuu huyo wa wilaya alimshukuru Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma pamoja na viongozi wengine wa Mahakama kwa kusikia ombi lao na kuwaongezea idadi ya Mahakimu watatu katika Mahakama ya wilaya ya Sengerema. Awali Mahakama hiyo ilikuwa na Hakimu moja tu.

Kuhusu ombi la Mkuu wa wilaya ya Sengerema la kuanzishwa kwa Mahakama ya pili ya wilaya kwenye wilaya hiyo, Jaji Kiongozi alisema Mahakama ya Tanzania itaangalia uwezekano wa kuanzisha masjala ndogo ya Mahakama ya wilaya ili kusogeza huduma kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Jaji Kiongozi anaendelea na ziara yake katika Mkoa wa Geita ambapo atamalizia katika wilaya za Bukombe na Chato.

 

 

 

Comments (0)

Leave a Comment