Post Details

JAJI MKUU AZINDUA VIKAO VYA KWANZA VYA RUFANI MASJALA NDOGO SUMBAWANGA

Published By:magreth.kinabo

Na Tiganya Vincent-Mahakama -Sumbawanga

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma tarehe 18  Septemba, 2023 amezindua vikao vya kwanza vya Mahakama ya Rufani katika Masjala ndogo Sumbawanga Mkoa wa Rukwa, hatua ambayo imelenga kusogeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi kwa ngazi hiyo ya Mahakama ya juu hapa nchini.

Akizungumza kabla ya uzinduzi huo ulioashiria kuanza kwa vikao hivyo, Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Sylvester Kainda alisema Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania umelenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma karibu yao na kwa gharama nafuu.

Alisema Masjala Ndogo ya Mahakama ya Rufani ya Sumbawanga imeanzishwa kufuatia Tangazo la Serikali Namba 520 la mwaka 2022 na kuongeza kuwa vikao hivi ndio vya kwanza.

Mhe. Kainda aliongeza kuwa kuanza kwa vikao vya Rufani katika Masjala Ndogo ya Sumbawanga itasaidia kutoa huduma kwa wakazi wa Mikoa ya Katavi na Rukwa ambao walikuwa wakifuata huduma hiyo mkoani Mbeya na kutumia gharama nyingi ikiwemo za malazi na nauli.

"Kuanzishwa kwa Masjala ndogo hapa Sumbawanga imekuwa masaada mkubwa kwa wananchi kwani mkazi kama wa Kijiji cha Mishamo wilayani Tanganyika alilazimika kusafiri umbali wa kilometa zaidi ya 500 kufuata huduma katika Masjala Ndogo ya Mbeya...wakati mwingine wapo wananchi walikuwa wakinipigia simu ya kuomba rufani zao zihahirishwe kwa sababu ya kukosa nauli" alisema.

Mhe. Kainda alisema katika kipindi cha wiki tatu jumla ya rufani 35 za mashauri ya aina mbalimbali zitapitia na kutolewa uamuzi miongoni yanahusu mauaji ikiwemo ya mtu aliyekuwa na uelemavu wa ngozi(albino) na nyingine zinahusu kupatikana na nyara za Serikali ikiwemo meno ya tembo na ubakaji.

Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga Mhe. Maira Kasonde alisema kuanza kwa vikao vya Rufani katika Kanda hiyo ni msaada mkubwa kwa wananchi kutokana  na mikoa ya Katavi na Rukwa kuwa na maeneo makubwa na baadhi ya vijiji kuwa pembezoni.

Alisema hali hiyo ilisababisha baadhi yao wananchi kulazimika kulala Mbeya wakati wakifuatilia Rufani zao na hivyo kuongeza gharama.

Mhe.Kasonde alisema kwa upande wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga imewapunguzia gharama pale walipokuwa wakitakiwa kupeleka nyaraka zilikuwa zinahitajiwa Mbeya.

Kikao hicho cha Mahakama ya Rufani, Masjala Ndogo ya Sumbawanga kitaongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji wa Rufani Mhe. Ferdinand Wambali, Jaji wa Rufani Panterine Kente na Jaji wa Rufani Zainabu Muruke.

 

Comments (0)

Leave a Comment