Post Details

MWENYEKITI MAHAKAMA SPORTS AWAITA WANAMICHEZO KAMBINI

Published By:faustine.kapama

Na Faustine Kapama-Mahakama

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) inatarajia kuanza kambi rasmi wiki ijayo ili kujiandaa na mashindano yajao ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayotarajia kufanyika kitaifa mkoani Iringa.

Mwenyekiti wa Timu hiyo Wilson Dede amewataka wanamichezo wote kutoka Mikoa yote nchini kufika katika Viwanja vya Shule ya Sheria kwa Vitendo Tanzania (Law School of Tanzania) kwa ajili ya kuanza  mazoezi kuelekea mashindano hayo.

“Wanamichezo wote wanatakiwa wawe Dar es Salaam kuanzia tarehe 22 Septemba, 2023, tayari kwa ajili ya kuanza mazoezi ya pamoja ili kumpa nafasi mwalimu kuchagua kikosi imara kitakachopeperusha vyema bendera ya Mahakama ya Tanzania SHIMIWI...

“.....nadhani unajua kilichotokea Tanga, tutaanzia tulipoishia mwaka jana na tutapiga pale pale kwenye mshono. Ndiyo maana tumeamua kuanza kambi mapema ili tuweze kuunda timu imara yenye ushindani katika michezo yote tutakayoshiriki,” alisema.

Michezo ambayo Mahakama Sports inatarajia kushiriki ni Kamba Wanaume, Kamba Wanawake, Mpira wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao, Karata, Tufe, Riadha Wanaume na Wanawake pamoja na Baiskeli.

Katika mashindano ya SHIMIWI yaliyofanyika mwaka jana jijini Tanga, timu ya Mahakama ya Tanzania ilizoa makombe saba baada ya kuibuka washindi katika michezo mbalimbali.

Michezo ambayo Mahakama Sports ilipata medali na makombe ni Kamba Wanawake walioibuka mshindi wa kwanza, Riadha Wanawake mita 3,000 mshindi wa kwanza, Tufe Wanawake mshindi wa kwanza, Kamba Wanaume walioshika nafasi ta pili, Mpira wa Miguu Wanaume walioshika nafasi ya pili na Bao Wanaume mshindi wa tatu.

Comments (0)

Leave a Comment