Post Details

RAIS MAGUFULI AMWAPISHA WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA

Published By:Mary C. Gwera

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewaapisha mawaziri wapya wa Wizara ya Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi na kuwataka kutekeleza wajibu wao mpya kwa kuzingatia viapo vya Maadili walivyoapa.

Rais Magufuli pia aliwaapisha Makamishna watano wa Jeshi la Polisi nchini pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Yahaya Simba ambao aliwateua hivi karibuni.

Akizungumza baada ya kuwaapisha Mawaziri hao pamoja na viongozi wengine, Rais Magufuli amewataka viongozi hao kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na kwa ushirikiano ili kuijenga Tanzania.

Aidha, Rais Magufuli amewataka Makamishna walioapishwa leo na Makamishna wengine kurekebisha kasoro ndogo zilizopo kwenye jeshi hilo ikiwemo watumishi wachache wanaokiuka maadili ya kazi kwa kujihusisha na uhalifu ili kujenga taswira chanya ya jeshi hilo kwa watanzania.

“Ninalithamini jeshi la polisi nchini kwa kuwa linafanya kazi nzuri, jirekebisheni”, alisema. 

Rais Magufuli pia amewataka viongozi wa jeshi hilo kutowakatisha tamaa kwa kutowaunga mkono askri wa wanapotekeleza majukumu yao kwa usahihi kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wakiwadhalilisha na kuwavunja moyo katika kazi yao.

Aidha, amewataka Majaji, Mawaziri, Makamishna wa Polisi, Makatibu wakuu pamoja na viongozi wengine wa serikali kutenda haki kwa watanzania na kuwataka viongozi hao kutanguliza mbele maslahi ya taifa  na kuhimiza umoja baina ya wananchi ili nchi ifanikiwe. 

Akizungumza kwenye hafla hiyo iliyofanyika leo Ikulu jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Prof. Ibrahimu Hamis Juma amewapongeza Mawaziri wa Katiba na Sheria na Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kumwelezea Prof. Kabudi kuwa ni kiongozi aliyeifahamu vizuri Mahakama ya Tanzania na dhana yake ya kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

 

Jaji Mkuu aliitaja baadhi ya mikakati ya Mahakama ya Tanzania ya kusogeza huduma karibu zaidi na wananachi kuwa ni ujenzi wa majengo ya Mahakama katika ngazi zote, uanzishwaji wa Mahakama inayotembea (Mobile Court) pamoja na matumizi ya Tehama katika kurahisisha upatikanaji wa haki.

Prof. Juma ameahidi kushirikiana na Waziri Mahiga katika kutekeleza jukumu la msingi la Mahakama la kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati kwa kuwa atakuwa ni kiungo kati ya wananchi na mhimili wa Mahakama.

Comments (0)

Leave a Comment