Post Details

WASAIDIZI WA SHERIA WA MAJAJI RUFANI WAFUNDWA MASHAURI YA UCHAGUZI

Published By:Mary C. Gwera

Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman amewataka Wasaidizi wa Sheria wa Majaji kutumia taaluma yao na kuzingatia umahiri na weledi katika uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi sambamba na kujiepusha na ushabiki wa kisiasa.

Akifungua mafunzo ya Wasaidizi wa sheria 39 wa Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania juu ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi hivi karibuni yaliyofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mh. Chande aliwaomba washiriki hao kuzingatia na kufuatilia mafunzo hayo kikamilifu ili wakayatumie katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Mkiwa kama wasaidizi wa Sheria wa Majaji ni vyema kutumia taaluma yenu vizuri na kuzingatia umahiri na weledi katika uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi na kujiepusha na ushabiki wa kisiasa,” alisisitiza Jaji Chande.

Aidha, Mhe. Chande aliwataka washiriki hao kufanya kazi kwa kuzingatia maadili, umakini na kujiamini katika uandishi wa hukumu hivyo wanalazimika kuendelea kujinoa ili kuendana na kasi ya mabadiliko na izingatwe kuwa wao ni msaada mkubwa kwa Wahe. Majaji katika utekelezaji wa majukumu ya utoaji wa haki. 

Kwa upande mwingine, Jaji Chande aliupongeza Uongozi wa Mahakama ya Tanzania na wa Chuo hicho kwa kuwa mstari mbele katika kufanikisha mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa mbalimbali wa Mahakama katika kushughulikia mashauri ya Uchaguzi.

Mpaka sasa Mahakama kwa kushirikiana na Chuo tayari imeshafanya mafunzo ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa Maafisa mbalimbali wa Mahakama ikiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu, Naibu Wasajili, Mahakimu Wakazi Wafawidhi lengo likiwa ni kuwawezesha kuyashughulikia kwa ustadi zaidi na kwa wakati.

Comments (0)

Leave a Comment