Post Details

JENGENI UTAMADUNI WA KUJIFUNZA MASUALA YA KISHERIA; JAJI MKASIMONGWA

Published By:Mary C. Gwera

Wakazi wa Jiji la Tanga na wananchi wote kwa ujumla wameshauriwa kujenga utamaduni wa kujifunza masuala ya kisheria ili kuweza kufahamu na kutambua haki zao.

Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Edson Mkasimongwa aliyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akitoa elimu ya sheria kwa wananchi/wateja wa Mahakama waliofika kupata huduma mbalimbali za kimahakama katika Kanda hiyo.

“Katika kipindi hiki ambacho watoto wetu watakuwa wamemaliza darasa la saba, wakati wakisubiria matokeo yao, ni vema wazazi mkapanga hata siku moja kuja nao hapa Mahakamani angalau na wao wakapata mawili matatu yanayohusu masuala ya sheria”, alisema Jaji Mkasimongwa.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliobahatika kupata elimu iliyotolewa na Mhe. Jaji waliipongeza Mahakama kwa kuanzisha mpango wa kuwaelimisha kuhusu masuala ya kisheria kuiomba Mahakama kuangalia namna ya kufanya lugha ya Kiswahili itumike kuandaa Mienendo ya kesi pamoja na Hukumu kuanzia ngazi ya Mahakama za Wilaya mpaka ngazi ya Mahakama ya Rufani.

Wananchi hao walitoa maoni yao juu ya kusambaza vipeperushi vya Mahakama vya kutosha ili kuwafikia watu wengi hasa wale waliopo vijijini.

Huu ni mwendelezo wa utoaji Elimu ya sheria kwa Umma, ambapo wananchi hao walipata elimu juu ya utaratibu wa ufunguaji wa Mashauri Mahakamani. Aidha, katika zoezi hilo, Mhe. Jaji Mkasimongwa aliambatana na Bi. Nakijwa Kachua, Msaidizi wa kumbukumbu wa Kanda hiyo.

Mahakama nchini imejiwekea utaratibu wa kutoa elimu ya sheria kwa wateja wake ili kuwawezesha wananchi kuwa na uelewa wa masuala na taratibu mbalimbali za kisheria zitakazowawezesha kujua nini cha kufanya pindi wanapotafuta huduma ya haki.

Comments (0)

Leave a Comment