Post Details

MAANA HALISI YA MAJENGO MAZURI IONEKANE KWA WADAU INAOWAHUDUMIA – JAJI KIONGOZI

Published By:LYDIA CHURI

Na Innocent Kansha Mahakama -Chunya

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amewahakikishia wananchi na wadau mbalimbali wa Mahakama kuwa Mhimili utaendelea kuwatendea haki wananchi kwa wakati ili maana halisi ya majengo mazuri ionekane kwa wadau inaowahudumia.

Akizindua jengo la Mahakama ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya jana Oktoba 9, 2020, Jaji Kiongozi alisema, Mahakama ya Tanzania inajenga majengo ya kisasa kwa sababu kubwa moja ambayo ni kuwarahisishia wananchi kupata huduma ya haki wanayostahili kwa wakati bila ubaguzi.

“Natoa rai kwa watumishi wa Mahakama, majengo haya ya kisasa na miundombinu bora iambatane na upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi, badilini mienendo na tabia ambazo zinakiuka miiko na maadili ya kazi za utumishi wa umma”, alisisitiza Jaji Kiongozi.

Mhe. Dkt. Feleshi aliwataka viongozi kuhakikisha kwamba watumishi wote wanatoa huduma nzuri zinazoendana na uzuri wa jengo hilo ili kutimiza azma hiyo aliwasisitiza kujiepusha na kauli mbaya kwa wateja na vitendo vya rushwa kwa wadau wanaowahudumia kwani rushwa ni adui wa haki.

Jaji Kiongozi aliongeza kuwa uboreshaji wa miundombinu ya majengo hautakuwa na maana endapo hautaenda sambamba na huduma rafiki zitolewazo na Mahakama ya Tanzania, kwa mwaka huu wa kimahakama 2020, Mhimili umeazimia kuboresha huduma zake ikiwa ni pamoja na kusikiliza na kuamua mashauri kwa wakati, utoaji wa nakala za hukumu na kutatua kero na malalamiko ya wananchi kwa wakati.

Mahakama ya Tanzania pia imeazimia kusimamia maadili ya watumishi kwani ni ukweli usiopingika kwamba mafanikio ya Taasisi hutokana na watumishi wachapakazi na wenye maadili, aliongeza Dkt. Feleshi.

Jaji kiongozi alisema, kuzinduliwa kwa jengo hilo la kisasa lililofungwa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pia litawarahisishia Mahakimu kusikiliza na kumaliza mashauri 250, idadi ambayo kila Hakimu katika Mahakama ya Wilaya anapaswa kumaliza katika kipindi cha mwaka mmojas.

“Ni imani yangu kuwa wananchi na wadau wetu wa Mahakama watapata mahitaji yao ya msingi kwenye mazingira bora kabisa wakati mashauri yao yanasikilizwa na hata wakati watakapokuwa wanasubiri kupata huduma”, aliongeza Jaji Kiongozi.

Mahakama ya Tanzania inathamini na kutambua mchango mkubwa wa wananchi wote wa Tanzania wanaolipa kodi ambayo inaiwezesha Serikali kutekeleza miradi ya kimkakati, ikiwemo majengo ya Mahakama, Ni matamanio ya Mahakama kwamba majengo haya yanayojengwa kwa fedha za wananchi yatatumika kutoa haki kwa kila Mtanzania na kwa wakati unaostahili, alisema Jaji Kiongozi.

Dkt Feleshi alisema, Wilaya ya Chunya ina sifa za kipekee katika Mkoa wa Mbeya katika Nyanja mbalimbali za kilimo, biashara, viwanda, ufugaji wa mifugo, uchimbaji wa madini na ina idadi ya wakazi zaidi ya laki 200,000 (laki mbili) Upatikanaji wa huduma bora za Mahakama hii unaenda kuunga mkono jitihada za kuleta maendeleo ya Wilaya ya Chunya na Taifa kwa ujumla.

Akizungumzia hali ya mashauri katika Mahakama ya Tanzania Jaji Kiongozi alisema, kwa mwaka huu kuanzia Januari mashauri yaliyosajiliwa kwenye kanzidata yaani mfumo wa JSDS II ni elfu 57,702, yaliyosikilizwa ni elfu 60,649, yaliyosajiliwa kwa njia ya mtandao (E – Filing) ni 14,184 na kwa upande wa mashauri ya jinai yaliyobakia hadi sasa ni 21,284

Awali Jaji kiongozi alikutana na Mkuu wa Wilaya ya Chunya pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ofisini kwake na kuwakumbusha watendaji hao wa serikali kuwa wana jukumu la kuipa ushirikiano Mahakama hasa pale wanapopanga mikakati ya kimaendeleo, uzoefu unaonyesha kuwa mara nyingi serikali imekuwa ikipanga mipango mingi ya kimaendeleo na kuanzisha Taasisi za kutoa huduma mbalimbali lakini Mahakama mara zote haipewi kipaumbele katika miradi hiyo.

Wakati huo huo Mkuu wa Wilaya ya Chunya Bw. Mayeka Simon Mayeka aliipongeza Mahakama na Serikali kwa jitihada za uboreshaji wa majengo ya Mahakama kwa ngazi mbalimbali nchini kuanzia Mahakama za mwanzo hadi Mahakama Kuu.

“Maboresho haya makubwa sasa yatasaidia kupunguza mlundikano wa mashauri hasa kwa Wilaya ya Chunya kwani katika kipindi hiki ambacho Mahakama inaendesha shughuli zake za utoaji haki kidijitali”, alisema.

Bw. Mayeka Simon Mayeka aliihakikishi Mahakama kuendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali katika ngazi ya Mkoa na Wilaya pale watakapo takiwa kufanya hivyo kwa yale mambo yote yaliyo ndani ya uwezo wa serikali ya Mkoa na Wilaya.

Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya Mhe. Dkt. John Utamwa alisema anaushukuru Uongozi wa serikali wa Wilaya ya Chunya kwa ushirikiano kwa kipindi chote kutokana na historia ya Mahakama wilayani Chunya toka mwaka 1968 kwa kuwapa mahala pa kutolea huduma za Mahakama hadi jengo la Mahakama lilipo kamilika.

“Mimi kama Jaji Mfawidhi wa kanda ya Mbeya nimeshuhudia ushirikiano mkubwa tuliopewa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Chunya tulitimiza majukumu yetu bila kubugudhiwa na kwa kipindi chote hatukupokea suala lolote linalohusiana na kuharibika kwa mahusiano yetu katika utendaji wetu”, aliongeza Jaji Mfawidhi Utamwa.

Wakati huo huo Mtendaji wa Mahakama Kuu kanda ya Mbeya Bw. Teoford Ndomba alisema, mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Chunya ulianza mwaka 2018 uliotekelezwa na kampuni ya PIM Innovators CO. Ltd, chini ya Msimamizi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa gharama za shilingi za kitanzania milioni 433/-.

 

Comments (0)

Leave a Comment