Post Details

JAJI BETHUEL MMILLA AFARIKI DUNIA

Published By:Mary C. Gwera

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAHAKAMA

 TAARIFA KWA UMMA

 

 JAJI BETHUEL MMILLA AFARIKI DUNIA

 

 

DAR ES SALAAM, 25.09.2020

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma anasikitika kutangaza kifo cha aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Marehemu Jaji Bethuel Mpakani Kasefu Mmilla aliyefariki dunia usiku wa Septemba 24, 2020.

Kwa mujibu wa Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi amesema, Marehemu Jaji Mmilla awali alilazwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo Septemba 23, 2020 alipokuwa akipatiwa matibabu na baadae alihamishiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Marehemu Jaji Mmilla alizaliwa Septemba 22, 1956 katika Wilaya ya Makete mkoani Njombe. Mnamo mwaka 1964 hadi 1970 marehemu alisoma shule ya Msingi Iniho Wilaya ya Makete.  Alijiunga na elimu ya Sekondari mwaka 1971 hadi 1974 katika Shule ya Sekondari Lugalo iliyopo mkoani Iringa, mwaka 1975 hadi 1976 aliendelea na elimu ya Sekondari katika Shule ya Sekondari ya Ilboru mkoani Arusha.

Aidha, Mwaka 1980 hadi 1983 marehemu Jaji Mmilla alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo alisomea Shahada ya kwanza ya Sheria (LLB). Alishiriki pia katika kozi mbalimbali fupifupi.

Marehemu Jaji Mmilla aliajiriwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) Machi 21, 1978 ambapo alifanya kazi hadi mwaka 1980. Mwaka 1983 alifanya kazi Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali. Mnamo Februari 1984 Marehemu Jaji Mmilla aliajiriwa na Mahakama ya Tanzania kama Hakimu Mkazi ambapo alifanya kazi katika vituo mbalimbali hadi Aprili, 1995.

Akiwa ndani ya Mahakama aliteuliwa pia kushika nafasi ya Usajili kazi aliyoifanya hadi Juni, 2000.  Kwa upande mwingine, mwaka 2000 marehemu aliteuliwa kuwa Katibu wa Tume ya Kurekebisha Sheria ambapo alifanya kazi hadi Juni, 2002.

Juni 05, 2002 aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa alimteua marehemu kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambapo aliitumikia Mahakama Kuu hadi Oktoba, 2012 alipoteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani hadi umauti unamfika.

Marehemu Jaji Mmilla atakumbukwa kwa uchapakazi na ushirikiano wa hali ya juu.

Kwa mujibu wa Bw. Nyimbi amesema kuwa msiba upo nyumbani kwa marehemu Mikocheni-Dar es Salaam na mipango ya mazishi itajulikana pindi itakapokamilishwa.

BWANA AMETOA, BWANA AMETWAA JINA LAKE LIHIMIDIWE.

 

Imetolewa na:-

Mary C. Gwera,

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano

MAHAKAMA YA TANZANIA            

Comments (0)

Leave a Comment