Post Details

TUMIENI TOVUTI ZA SERIKALI KWA MANUFAA, KABUNDUNGURU

Published By:Mary C. Gwera

Mtendaji Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru amewataka Maafisa Utumishi na Tawala wa Mahakama kutumia vyema tovuti rasmi za kiserikali zenye miongozo mbalimbali ya kiutendaji kazi itakazowawezesha kufanya kazi kwa ufanisi.

Akifungua rasmi kikao kazi cha siku mbili cha Maafisa hao mapema Septemba 03 kinachofanyika katika Ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam, Bw. Kabunduguru alisema kuwa maamuzi yoyote yanayofanywa na Kiongozi lazima yazingatie miongozo ya kisheria na sababu za maamuzi hayo  ni lazima zifuate utaratibu stahiki.

“Nataka muwe watawala wenye kufanya kazi zenu kwa umakini mkubwa kwa kuzingatia uweledi wa taaluma zenu, acheni kutumia mitandao ya kijamii badala yake someni tovuti rasmi za kiserikali kuna miongozo na mambo mengi mazuri ya kuwaongezea ujuzi wa kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa”, alisisitiza Mtendaji Mkuu.

Aliwataka pia kuhakikisha wanakuwa na nyaraka zote muhimu za sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ya kazi zenu itawasaidia kujua taratibu za majukumu yenu ya kuwaongoza watumishi wenzenu na kuwaongezea uwezo wa kupata maarifa ya ziada, alieleza Mtendaji Mkuu.

Aidha, Bw. Kabundunguru aliongeza kuwa matarajio ya Mahakama baada ya kumalizika kwa kikao kazi hicho ni kutumika kama suluhisho la kupanga mikakati ya namna bora ya kusimamia na kuboresha baadhi ya mambo kama vile usimamizi wa rasilimali watu ikihusisha mahudhulio, maadili na mahusiano kazini, miundo ya maendeleo ya utumishi, upimaji wa utendaji kazi unaozingatia taratibu zilizowekwa.

Maeneo mengine aliyoyasisitiza Mtendaji Mkuu ni uwasilishaji wa nyaraka kwa kuzingatia maelekezo, kuwasilisha maombi ya watumishi baada ya kufanya upembuzi yakinifu, usimamizi madhubuti wa kumbukumbu na nyaraka za kitaasisi na usimamizi madhubuti wa miundombinu, vyombo vya usafiri na mali nyingine za Umma.  

Kwa upande mwingine, Mtendaji Mkuu huyo aliwasisitiza Maafisa hao kuzingatia na kuendeleza ushirikiano na Mihimili mingine ya Serikali katika kutimiza majukumu yao.

“Tafuteni namna bora ya kufanya kazi na kupunguza malalamiko, Mahakama kama muhimili upo huru na unajitegemea katika kutimiza majukumu yake ya kikatiba, ila hauwezi kufanya kazi peke yake bila ushirikiano na taasisi zingine, tambueni kuwa Wakuu wa Wilaya na Mikoa ni wenyeviti katika kamati za maadili ya watumishi wa Mahakama kwa kupitia Sheria na. 4 ya mwaka 2011 ya uendeshaji wa Mahakama,” alisisitiza.

Hata hivyo, Bw. Kabundunguru alieleza kuwa anatambua changamoto mbalimbali zinazoikabili Mahakama ikiwa ni pamoja na uhaba wa miundombinu hasa ya majengo kwa baadhi ya maeneo ya kazi ila aliwahakikishia kuwa Mahakama itaendelea kuboresha miundombinu ya majengo kwa kukarabati na kujenga majengo mapya kwa awamu na hatimae kumaliza changamoto hiyo.

Kwa upande mwingine, Bw. Kabunduguru alisema kazi kubwa imefanyika kwenye usanifu, ujenzi pamoja na usimikaji na usimamizi wa mifumo ya mbalimbali ikiwemo mfumo wa kuratibu na kusimamia uendeshaji wa mashauri (JSDS II), ambao umerahisisha upatikanaji wa Takwimu na kuongeza uwajibikaji na uwazi kwenye mwenendo wa mashauri na pia kuongeza imani ya wadau na umma kwa Mahakama.

Mtendaji Mkuu alizungumzia juu ya Mpango Mkakati mpya wa Mahakama ya Tanzania utakaoanza mwaka 2020/2021 hadi 2024/2025 ambao utaendeleza mikakati ya kuboresha miundombinu na kuongeza matumizi ya TEHAMA kuboresha zaidi shughuli za kimahakama.

 

Comments (0)

Leave a Comment