Post Details

TOENI MAAMUZI YA KESI ZA UCHAGUZI KWA UWAZI HAKI NA BILA UPENDELEO: JAJI MKUU

Published By:LYDIA CHURI

Na Lydia Churi-Mahakama, Morogoro

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Majaji na Mahakimu kutoa maamuzi ya kesi zinazohusu uchaguzi kwa uwazi, haki na bila upendeleo wowote ili kulinda heshima ya Mhimili wa Mahakama.

Akifungua mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani yaliyoanza leo mjini Morogoro, Jaji Mkuu amesema ni uwazi na kufuata sheria tu ndiyo vitaongeza imani ya wananchi kwa Jaji au Hakimu na kwa Mahakama kwa ujumla.

“Kazi yetu na maamuzi yetu yaongozwe na sheria pamoja na ushahidi unaotolewa mbele yetu na si vinginevyo”, alisisitiza.

Aliwataka Majaji na Mahakimu kufahamu kuwa mashauri yanayotokana na uchaguzi Mkuu hutumiwa na wananchi katika kupima na kutathmini utendaji kazi wa Mahakama ya katika maeneo mbalimbali ya utoaji haki. Alisema katika kipindi cha uchaguzi wananchi hupima uhuru wa Jaji au Hakimu mmoja mmoja na pia hupima uhuru wa Mahakama kwa ujumla.

“ingawa wananchi wengi huwa hawafuatilii mashauri ya kawaida ya jinai na madai, hali hubadilika wakati wa mashauri ya uchaguzi ambapo hufuatilia taratibu zote zinazohusu kesi za uchaguzi”, alisema.

Akizungumzia mafunzo hayo, Jaji Mkuu amewataka Majaji kuibua maeneo ya uchaguzi yanayohitaji maboresho kwa lengo la kuboresha kanuni hizo ili mashauri ya uchaguzi yamalizike kwa wakati na hivyo kujenga Imani ya wananchi kwa Mahakama.

Alisema Majaji ni viongozi hivyo maamuzi yao hushawishi kuboreshwa kwa sheria au kubadilishwa kwa sera zinazohusu masuala ya sheria na haki.

“Tuchukulie mafunzo haya kama fursa ya pekee ya kuibua maeneo ya uchaguzi ambayo yanahitaji maboresho Zaidi, alisema.

Alisema mafunzo hayo yatawasaidia Maafisa hao wa Mahakama kuwa katika hali ya utayari wa kupokea, kusikiliza na kumaliza mashauri yote ya uchaguzi ndani ya muda mfupi na pia mafunzo hayo ni muhimu katika uimarishwaji wa uchaguzi ulio huru na wa haki.

Mafunzo ya nmana bora ya uendeshaji wa kesi za uchaguzi yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika kwa nyakati tofauti yanawahusisha Maafisa wa Mahakama wa ngazi mbalimbali wakiwemo Majaji, Wasajili, Mahakimu na Wasaidizi wa Sheria wa Majaji.

 

 

 

Comments (0)

Leave a Comment