Post Details

JAJI MKUU ASISITIZA USHIRIKIANO WA MAHAKAMA NA SERIKALI

Published By:LYDIA CHURI

Na Lydia Churi-Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemtaka Hakimu Mkazi Mfawidhi mpya wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga Mhe. Mary Peter Mrio kushirikiana na viongozi wa mkoa huo anapotekeleza majukumu yake ya utoaji haki.

Akizungumza wakati wa hafla ya kumkabidhi hati ya uteuzi (Instrument) Hakimu huyo ambaye alimteua hivi karibuni kuwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga, Jaji Mkuu amesema mihimili yote ya dola haina budi kushirikiana bila ya kuingiliana mipaka yake.

“Zingatia Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania unapotekeleza majukumu yako ya kila siku na pia uisome na kuifahamu vizuri Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025”, alisisitiza Jaji Mkuu.

Alisema Mahakama ya Tanzania imefanya na inaendelea kufanya maboresho mbalimbali ya huduma zake hivyo Hakimu huyo hana budi kuhakikisha maboresho hayo yanaelezwa kwa wnanchi walio wengi ili waweze kufahamu huduma mbalimbali zinazotolewa na Mahakama.

“Mambo mengi mazuri tumeyafanya hivyo tunapaswa kuyaeleza,    mitandao ya kijamii itumike zaidi kuwaelimisha wananchi juu ya mipango mizuri ya Mahakama”, alisema.

Aidha, Jaji Mkuu alimtaka Mhe. Mrio kujiepusha na migongano inayoweza kutokea katika kutekeleza shughuli za utoaji haki na zile za Mahakama za kiutawala.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga, Mhe. Mrio alikuwa ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.

Comments (0)

Leave a Comment