Post Details

WADAU WAKUMBUSHWA UMUHIMU WA KULINDA HAKI YA MTOTO

Published By:LYDIA CHURI

Na Innocent Kansha – Mahakama, Dodoma

Vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto ni mambo yanayopaswa kukemewa kwa nguvu zote katika jamii kwa kuwa vinachangia kwa kiasi kikubwa mmomonyoko wa maadili.

Akifungua mafunzo ya wadau ya namna bora ya uendeshaji na uboreshaji wa mfumo wa haki jinai kwa watoto kuhusu unyanyasaji wa kijinsia, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma Mhe. Mustapher Siyani amesema

Vitendo hivyo pia vinaweza kuongezeka kutokana na watu wengi kuamini katika ushirikina.

“Ni matarajio na matamanio yetu kuwa baada ya mafunzo haya wadau na maafisa wa Mahakama watakuwa wameelewa sheria na kanuani za namna nzuri ya kushughulikia mashauri ya watoto kwa kuzingatia masilahi bora ya mtoto na kulinda haki zao”, alisema Jaji mfawidhi.

Alisema mfumo wa haki jinai kwa mtoto nchini unakua kwa kasi kubwa hivyo anaamini mafunzo hayo wadau na washiriki watapata ujuzi na uzoefu wa kutosha katika kusaidia namna bora ya kuendesha mashauri ya watoto.

‘Ugumu wa taratibu mbalimbali za uendeshaji wa mashauri ya watoto unachangiwa na mila na desturi, wadau kutopitia hadidu rejea mbalimbali na maamuzi ya Mahakama ya Juu inapotoa miongozo ya namna sahihi ya uendeshaji wa mashauri ya watoto’, alisisitiza.

Jaji mfawidhi aliwataka washiriki kuzingatia mambo muhimu katika uendeshaji wa mashauri ya watoto ikiwemo mila na desturi, malezi, makuzi na misingi ya dini kwani ni baadhi ya mambo mtambuka katika utoaji wa haki.

Mhe. Siyani aliwakumbusha washiriki wajibu wao wa kuzingatia utawala wa sheria katika kutatua changamoto zitokanazo na matendo haya ya kidhalimu yanayodumaza ustawi wa mtoto ikiwemo kutoa elimu kwa watoto ili waweze kuripoti kwa viongozi vitendo vyovyote vinavyoashiria unyanyasaji wa kijinsia kama sheria ya mtoto inavyoelekeza.

Awali akitoa neno la utangulizi, Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo na Mratibu Mkuu wa Mafunzo hayo Bi. Mwanabaraka Mnyukwa alisema mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo ya uendeshwaji wa mashauri ya mtoto kwa wadau wa sekta ya sheria nchini yanayoratibiwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Chama cha Mawakili Tanganyika-TLS. Awali mafunzo hayo yalikuwa yakiratibiwa kwa kushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania na Shirika la umoja wa mataifa linalojishughulisha na masuala ya watoto (UNICEF).

Tanzania imeingia katika makubaliano kadhaa ya kimataifa na ya kikanda juu ya haki na makuzi ya mtoto ikiwa ni pamoja na kuwa sehemu ya azimio la kimataifa la haki za binadamu, mikataba mbayo imepelekea kwa kiasi kikubwa kuboresha utekelezwaji wa masuala mbalimbali yanayozunguka maslahi ya mtoto.

Mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Dodoma yaliwashirikisha maafisa wa Mahakama, Ustawi wa jamii, waendesha mashitaka na Chama cha Mawakili Tanganyika.

 

 

 

 

 

 

Comments (0)

Leave a Comment