Post Details

MASHAURI YA UCHAGUZI YAAMULIWE KWA UWAZI, UTULIVU NA KUJIAMINI- JAJI SIYANI

Published By:LYDIA CHURI

Na Innocent Kansha – Mahakama Dodoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dodoma Mhe. Mustapher Siyani amewataka Naibu Wasajili wa Mahakama ya Tanzania kuamua mashauri yatakayotokana na uchaguzi Mkuu kwa uwazi, utulivu na kujiamini.

Akifungua awamu ya pili ya mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa baadhi ya Waheshimiwa Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji Siyani amesema kuwa mashauri ya Uchaguzi yana maslahi kwa Umma na hivyo yanapaswa kushughulikiwa kwa haraka na umakini kwa kuwa lengo la Mahakama ni kuhakikisha kuwa haki za wananchi ikiwemo haki ya kuchagua kiongozi wanayemtaka inalindwa.

“Uchaguzi ni miongoni mwa mambo yanayotumia rasilimali nyingi za Taifa katika kulitekeleza jukumu hilo la kidemokrasia, hivyo ni imani yangu kuwa mafunzo haya yatachangia kuleta matokeo chanya katika kupokea na kusikiliza mashauri yatakayohusu uchaguzi muda utakapofika”, alisema.

Alisema ili uchaguzi uwe huru na wa haki ni dhahiri Mahakama haiwezi kujitenga na mchakato mzima, siyo tu kwa maisha ya kila mwananchi bali pia kwa ustawi wa nchi na hivyo Mahakama ni  mdau  na muhimu katika mchakato mzima wa uchaguzi ujao.

“Mahakama ndicho chombo kilichokasimishwa mamlaka ya kutoa haki kwa mujibu wa Ibara ya 107 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mahakama hutumika kutafsiri sheria mbalimbali, miongoni mwa sheria hizo ni sheria zote zinazosimamia masuala uchaguzi”, aliongeza Jaji Siyani.

Alisema mara nyingi wakati wa uchaguzi mkuu, huwa kuna joto la uchaguzi na nyakati hizo mashauri mbalimbali ya uchaguzi hufunguliwa mahakamani, kwa kuzingatia umuhimu wa mashauri hayo ni wajibu wa Mahakama kuyapa kipaumbele na uharaka unaostahili. “Ni lazima tuwe wazalendo kwa kiasi kikubwa pindi tunapoliendea jambo hili muhimu kwa mustakabali wa nchi yetu”, alisisitiza.

Jaji Siyani aliongeza kuwa Mahakama inao wajibu wa kuona mashauri yanayohusu uchaguzi yanayofunguliwa mahakamani yanaisha kwa wakati na haki inapatikana bila uvunjifu wa amani.

Mafunzo haya ni muendelezo wa mafunzo yaliyoanza kutolewa kwa Majaji wafawidhi na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuhusu namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu. 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Comments (0)

Leave a Comment