Post Details

VIKAO VYA MAHAKAMA YA RUFANI VYAANZA KUFANYIKA SHINYANGA

Published By:LYDIA CHURI

 Emmanuel Oguda-Mahakama, Shinyanga

Vikao vya Mahakama ya Rufani, kwa mara ya kwanza vimeanza kufanyika Shinyanga baada ya kufunguliwa rasmi kwa huduma hizo na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma jana.

Ufunguzi huo umefanyika kwenye ofisi za Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga kupitia gwaride maalum lililoandaliwa na Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga na kukaguliwa na Mhe. Jaji Mkuu.

Kufuatia ufunguzi huo, wananchi wa Mkoa wa Shinyanga sasa wataanza kupata huduma za Mahakama ya Rufani. Kupitia Tangazo la Gazeti la Serikali No. 579 la tarehe 24/7/2020, jengo la Mahakama Kuu Shinyanga, limetangazwa kuwa ni Masjala Ndogo ya Mahakama ya Rufani.  Kila mwaka, Mahakama ya Rufani itakuwa na vikao katika jengo la kanda ya Shinyanga.  

Katika vikao hivyo Jumla ya mashauri 29 yanatarajiwa kusikilizwa na Majaji wa Mahakama ya Rufani akiwemo Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe Prof. Ibrahim Hamis Juma pamoja na Majaji wengine ambao ni Mhe. Charles Mwambegele, Mhe. Augustino Mwarija na Mhe. Rehema Kerefu.

Aidha, kikao hicho cha kwanza cha Mahakama ya Rufani kitasikiliza mashauri ya aina mbalimbali yakiwemo; Maombi ya Madai 5, Rufaa ya Madai moja, na Rufaa za Jinai 23.

Jengo la Mahakama kanda ya Shinyanga lilizinduliwa rasmi Agosti 7 mwaka huu na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma baada ya kukamilika kujengwa Mwaka 2015 kwa gharama za shilingi bilioni 3.9 ambazo ni fedha za ndani.

Comments (0)

Leave a Comment