Post Details

MABORESHO YA MIUNDOMBINU NI CHACHU YA UTOAJI HAKI KWA WAKATI

Published By:LYDIA CHURI

Na Innocent Kansha – Mahakama Logindo.

Mahakama ya Wilaya ya Longido imefanikiwa kusikiliza na kuyatolea uamuzi mashauri ya Jinai na Madai 72 kati ya mashauri 90 yaliyosajiliwa katika kipindi cha Januari hadi Julai 31 mwaka huu.

Akizungumza na Maafisa Habari wa Mahakama ya Tanzania, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Longido Mhe. Aziza Emily Temu alisema mashauri hayo yamesikilizwa na kumalizika kati ya mwezi Januari na Julai, mwaka huu.

“Mashauri yaliyobaki mwezi Desemba 2019 yalikuwa ni 128 yaliyosajiliwa kati ya Januari na Julai mwaka huu ni mashauri 90, tumesikiliza na kumaliza jumla ya mashauri 72 na kubakiwa na mashauri 146”, alifafanua Mhe. Temu.

Kwa mujibu wa Hakimu Mfawidhi huyo, asilimia kubwa ya mashauri yanayofunguliwa kwenye Mahakama hiyo ni ya kukutwa na Dawa za kulevya hasa Bangi na Mirungi, Mauaji na mashauri ya madai kwa uchache.

Alisema mashauri yanayohusu kukutwa na dawa za kulevya mirungi na bangi, yanachangiwa na Wilaya ya Longido kuwa mpakani mwa Tanzania na Kenya hivyo kutumika kama korido ya kusafirisha mihadarati.

Kuhusu matumizi ya Tehama yalivyochangia utoaji haki kwa wakati kwenye Mahakama hiyo, Mhe. Temu alisema mashauri yote yaliyosajiliwa kuanzia mwaka 2012 yameingizwa na kuhuishwa kwenye mfumo wa utunzaji kumbukumbu za kimahakama (JSDS II) ambapo kazi hii imechagiwa na kufungiwa mkongo wa Taifa wa mawasiliano.

“Imepelekea urahisishaji wa upatikanaji wa takwimu, kutunza taarifa za mashauri kwa haraka, kutuma taarifa za ujumbe mfupi kwa wadaawa ili kuwafahamisha hatua mbalimbali za mashauri yao na kuonyesha dhahiri shairi tuko katika Mahakama ya kimtandao zaidi”, alisema Hakimu huyo.

“Mahali pazuri pa kufanyia kazi panaleta ufanisi mzuri kiutendaji kwa maana ya utoaji haki kwa wakati na kuonekana haki ikitendeka, nawasihi wadau wetu kurejesha imani kwa Mahakama yao, tumejiwekea mipango madhubuti ya kuhakikisha tunawahudumia kwa weledi kwa kufuata kanuni na misingi ya kisheria” alisisitiza Mhe. Temu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Longido mkoani Arusha Mh. Frank James Mwaisumbe alisema wananchi wana fursa ya kuitumia Mahakama yao iliyosongezwa karibu na yenye hadhi, wafahamu kuwa ipo kwa ajili yao ili kupata haki na si vinginevyo na hasa jinsia ya kike.

“Uwepo wa Mahakama hii ya kisasa itakuwa suluhisho la utatuzi wa migogoro kwenye jamii hii ya kifugaji hasa unyanyasaji wa kijinsia kwa akina mama wanaohesabika kama watoto kwenye koo za Kimaasai, hivyo itasaidia kutatua matatizo yaliyokuwa yakiamriwa kijadi na kuacha manung’uniko kwa ustawi wa jamii”, alisema Mkuu wa Wliaya.

Mh. Mwaisumbe alisema serikali itaendelea kutoa elimu ikishirikiana na Mahakama ili wanajamii waelewe umuhimu wa chombo hiki na jinsi kinavyotenda kazi zake, na sasa itakuwa jibu la mambo yote yanayokwenda kinyume na taratibu za kisheria.

 

 

 

 

 

 

 

Comments (0)

Leave a Comment