Post Details

MAJAJI SITA WAPYA MAHAKAMA YA RUFANI WAAPISHWA

Published By:faustine.kapama

Na Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 23 Mei, 2023 amewaapisha Majaji sita wapya wa Mahakama ya Rufani aliowateua hivi karibuni.

Hafla hiyo ya uapisho imefanyika katika Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa wa Serikali na Mahakama. Majaji hao wamekuwa viongozi wa kwanza kuapishwa na Rais Samia kwenye jengo jipya la Ikulu tangu lilipozinduliwa tarehe 20 Mei, 2023.

Majaji hao ni aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Zainab Goronya Mruke na aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dar es Salaam, Mhe. Leila Edith Mgonya.

Wengine ni aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Shule ya Sheria Tanzania, Mhe. Dkt. Benhajj Shabaan Masoud na aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Amour Said Khamis.

Kadhalika, aliapishwa aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson John Mdemu na aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Agnes Zephania Mgeyekwa.

Viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe, Prof. Ibrahim Hamis Juma.

Wengine ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani.

Kulikuwepo pia na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, watumishi mbalimbali wa Mahakama wakiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel na ndugu na jamaa wa viongozi hao walioapishwa.

Tukio hilo pia liliambatana na uapisho wa Mwenyekiti wa Baraza la Maadili, Mhe. Rose Teemba, ambaye ni Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Baada ya uapisho huo, viongozi hao walikula kiapo cha uadilifu kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Sivangilwa Mwangesi.

Akizungumza baada ya kuwaapisha viongozi hao, Rais Samia aliahidi kuendelea kuiwezesha Mahakama kwa kuipatia nguvu kazi ya kutosha ili kuharakisha mchakato mzima wa utoaji haki kwa wananchi.

Mhe. Dkt, Samia alisema ataongeza jopo moja la Majaji wa Mahakama ya Rufani ili yafikie kumi (10), hatua itakayosaidia kuongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri na utoaji wa uamuzi.

Alielezea furaha yake baada ya kuona wale aliowateua kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani ni miongoni mwa wale aliowateua kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na wamekuwa wakitimiza majukumu yao kikamilifu.

“Nakupongeza Jaji Mkuu kwa kupata timu mpya. Kwa majaji wapya, hongereni sana kwa kupata uteuzi huu na kuapa. Kuna Majaji hapa niliwapandisha mwenyewe kutoka huko walikokuwa kwenda Mahakama Kuu na leo wale wale nawaapisha kwenda Mahakama ya Rufani. Hii inanipa faraja kundi hili linachapa kazi sawa sawa,” alisema.

Naye Waziri Mkuu aliwaeleza Majaji hao kuwa Watanzania wanamategemeo makubwa kutoka kwao na wanahamu ya kutendewa haki katika mahitaji yao mbalimbali. “Sisi hatuna mashaka na nyinyi, utendaji wenu uliotukuka tunauona, uadilifu na uaminifu katika kufanya kazi za utoaji haki,” alisema.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge alieleza kuwa kama mwakilishi wa wananchi wanatamani kuona hukumu zinatolewa kwa haraka ili wapate haki yao. Alieleza kuwa Bunge litakuwa tayari kuzifanyia marekebisho sheria zile zinazoleta changamoto katika utendaji wa Mahakama ili wananchi wapate haki zao haraka.

Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Mkuu wa Tanzania alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia kwa kuiongezea nguvu kazi Mahakama katika upande wa Mahakama ya Rufani, kwani ongezeko la Majaji hao linaenda kupunguza mzigo wa kila jopo katika kusikiliza na kuamua mashauri.

Mhe. Prof. Juma aliwakumbusha Majaji hao majukumu yao katika Mahakama ya Rufani ambayo ni kusikiliza na kuamua mashauri, hivyo akawahimiza kutekeleza kazi hizo kwa wakati ili wananchi wapate haki zao na pia kuchochea uchumi.

Rais Samia aliwateua Majaji hao sita tarehe 28 Aprili, 2023, hivyo kuongeza idadi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani kutoka 25 waliokuwepo hadi 31, bila kujumlisha Jaji Mkuu.

Comments (0)

Leave a Comment