Published By: | Mary C. Gwera |
---|
Na Arapha Rusheke, Mahakama Kuu Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama nchini, Mhe.Prof.Ibrahim Hamis Juma ameahirisha kikao cha siku mbili cha Baraza Kuu la wafanyakazi wa Mhimili huo kilichokuwa kikifanyika katika Ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma.
Akihairisha kikao hicho leo tarehe 19 Mei, 2023, Jaji Mkuu ameahidi hoja zote zitafanyiwa kazi na kufuatiliwa na kuhakikisha kwamba yanafanyiwa kazi kwani lengo ni kuboresha mazingira ya utoaji huduma sambamba na kuboresha maslahi watumishi kwa ngazi zote za Mahakama.
“Mkutano wetu wa siku mbili umekuwa na masomo mengi sana. Mimi naamini kila mmoja wetu amejifunza kitu kwa sababu tumekuja kwa nia ya kusikilizana, kujifunza changamoto mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali na kuna mambo mengi sana ambayo tumejifunza. Mimi binafsi naweza kusema nimejifunza mengi sana,’’ amesema Jaji Mkuu.
Miongoni mwa maazimio yaliyofikiwa katika kikao hicho ni pamoja na Watumishi wa Mahakama wapatiwe wapatiwe mafunzo ya msingi (basic knowledge) ya TEHAMA na matumizi ya mifumo ya KITEHAMA iliyopo mahakamani katika utoaji haki kwa kutumia mtaala ulioandaliwa ili wasaidie Mahakama ya Tanzania kuwa sehemu ya dunia ya kidijitali na uchumi wa maarifa.
Azimio lingine ni watumishi wanaokaribia kustaafu wapatiwe mafunzo kila robo mwaka na taarifa ya utekelezaji wake isambazwe kwenye Kanda zote.
Lingine, ripoti ya utafiti uliofanywa na REPOA kuhusu kuridhika kwa watumiaji wa huduma za mahakama (court user satisfaction survey) ya mwaka 2023 itakapochapishwa, itafsiriwe kwa Kiswahili na isambazwe kwa watumishi wote ili waisome na kujipima utendaji wao.