Post Details

IJA YAWAJENGEA UWEZO WAJUMBE WA MAMLAKA YA UDHIBITI WA HUDUMA ZA MAJI NA NISHATI ZANZIBAR (ZURA) KUH

Published By:Mary C. Gwera

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kimefungua mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo wa kanuni na mbinu za usuluhishi Wajumbe wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA).

Mafunzo hayo ya siku tano yalioyanza mapema wiki hii katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto mkoani Tanga, yanaratibiwa na Mkuu wa Chuo hicho, Mhe. Jaji, Dkt. Paul Kihwelo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mhe. Jaji Dkt Kihwelo alisema kuwa, mafunzo haya yamelenga kuwajengea uwezo wajumbe wa Bodi na Viongozi wa ZURA ili waweze kufanya kazi zao kwa weledi na kwamba ana matumaini makubwa kuwa mara baada ya mafunzo haya washiriki watakuwa na uelewa mpana zaidi wa kanuni na mbinu mbalimbali za usuluhishi.

“Chuo kimeandaa wakufunzi waliobobea katika eneo la Usuluhishi ili kuipa ZURA mafunzo yatakayokidhi haya na uhitaji katika utekelezaji wa majukumu yao,” alieleza Mkuu huo wa Chuo.

 

Mhe. Jaji Kihwelo alisema kuwa wakufunzi hao wana uzoefu huku akiwataja kuwa ni pamoja na Mh. Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Chande Othman  ambaye ana uzoefu wa kutosha katika eneo la usuluhishi kwa ngazi ya  kimataifa.

 Wengine ni Mh. Jaji John Mroso (Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa) na Mh. Jaji Teemba (Jaji Mstaafu Mahakama Kuu) ambaye ni mwanzilishi wa Kituo cha Usuluhishi nchini, akihudumu kama Jaji Mfawidhi wa Kituo hicho.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman alisema kuwa, lengo la kesi kwenda kwenye usuluhishi ni kurudisha uhusiano mwema kati ya pande mbili zenye mgogoro ili kuwawezesha kutatua mgogoro wao.

“Kuna umuhimu wa mgogoro kusuluhishwa na wenye mgogoro wenyewe na sio mtu wa nje, na ili  usuluhishi ufanikiwe lazima wenye mgogoro waingie kwenye usuluhushi wakiwa tayari kutoa na kupokea kwa sababu ukiingia huko suala la kushinda ama kushindwa linawagusa wote tofauti na mahakamani ambapo mmoja hushinda na mwingine hushindwa bila kusahau kuwa ni miongoni mwa njia za utatuzi wa migogoro” alieleza Mhe. Jaji Mstaafu Chande.

Pia Jaji Mkuu Mstaafu huyo alisema pia “sheria za nchi zetu mbili pamoja na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara 107 (a) ibara ndogo 2 (d) inatamka katika msingi wa utoaji haki ni kutatua migogoro kwa njia mbadala na ndio maana kwenye mashauri ya kazi kuna njia mbadala za kwenda kwenye Mahakama za usuluhishi (CMA).

 

Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Chande aliongeza kuwa, “kwenye masuala la talaka na ndoa kabla hujaletewa mashauri mahakamani lazima uende kwenye bodi ya usuluhishi na ni njia mbadala ya kuweza kutatua migogoro hiyo kwa njia ya haki mtu kupata haki kwa sababu haki haipatikani Mahakamani pekee.”

Kwa upande wake Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, Mhe. Jaji Rose Teemba  ambaye pia ni Mwanzilishi wa kituo cha Usuluhishi nchini alisema kuwa kituo hicho kilianzishwa rasmi kwa ajili ya mashauri ya madai yanayopelekwa Mahamakani kwa kutambua kwamba sheria inataka usuluhishi ufanyike kabla ya shauri halijaingia kusikilizwa rasmi.

Hali hii ilipelekea Uongozi wa Mahakama kuanzisha kituo hicho ili kuwe na wataalamu ambao ni Wahe. Majaji wataokuwa wakifanya kazi hiyo ya usuluhishi kama kazi za kila siku kutokana na ukweli kwamba Wahe. Majaji waliopo kwenye vituo vyao wamekuwa wakifanya kazi nyingi kwa wakati mmoja.

 

Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) Bw. Ally Abood Mzee Mjumbe alisema wao wamefarijika kupata fursa ya kuhudhuria mafunzo hayo na wana matarajio makubwa kuwa watatoka wakiwa wameiva vyema katika eneo hili muhimu na hivyo kuwawezesha kutatua migogoro iliyopo na itakayojitokeza kwa weledi mkubwa.

Miongoni katika faida za Usuluhishi ni pamoja na kusaidia kupunguza mlundikano wa mashauri Mahakamani, kujenga mahusiano mazuri baina ya wadaawa na kupunguza gharama za kesi za madai.

Mafunzo haya kwa wajumbe wa Bodi na Viongozi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), ni mfululizo wa mafunzo ya namna hiyo kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati, Maji na Mafuta, Tanzania Bara (EWURA) kuendeshwa na Chuo cha IJA kwa mafanikio makubwa mnamo mwaka, 2017.

 

Comments (0)

Leave a Comment