Post Details

MWILI WA JAJI BONGOLE KUZIKWA JUMANNE WILAYANI ROMBO

Published By:LYDIA CHURI

Na Lydia Churi -Mahakama

Mwili wa aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora Mhe. Salvatory Benedict Bongole unatarajiwa kuzikwa siku ya Jumanne tarehe 21/7/2020 katika kijiji cha Shimbi Kati wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.

Mwili wa Marehemu Jaji Bongole uliagwa jana katika Ibada iliyofanyika nyumbani kwake, Mtaa wa Ikulu, Cheyo A mkoani Tabora na baadaye kusafirishwa kwenda wilayani Rombo kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika siku ya Jumanne.    

Marehemu Jaji Salvatory Bongole alifariki dunia Jumatano usiku, Julai 15, 2020 baada ya kuugua ghafla nyumbani kwake.

Wasifu wa Marehemu Jaji Salvatory Bongole

Marehemu Jaji Bongole alizaliwa tarehe 6/4/1964 katika Kijiji cha Shimbi Kati Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro Tanzania. Januari 1975 hadi Novemba 1981 alisoma shule ya Msingi Kwandele.

Alijiunga na masomo ya sekondari Uru Seminari kuanzia mwaka 1982 hadi 1985 alipohitimu kidato cha nne. Mnamo Mei 1988 hadi Juni1989 aliendelea na masomo ya kidato cha tano hadi cha sita UrU Seminari na Juni 1988 hadi Juni 1989 alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Oljoro na Makuyuni.

Septemba 1989 alijiunga na Chuo kikuu Dar es salaam akisoma Shahada ya kwanza ya Sheria na kuhitimu Juni 1993.

Mnamo 10/6/1994 Mhe. Jaji Bongole aliajiriwa na Mahakama ya Tanzania kama Hakimu Mkazi Daraja la III.

Tarehe 16/10/2000 aliteuliwa kuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Mtwara. Mnamo tarehe 2/8/2000 aliteuliwa kuwa Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Nyumba Mkoa wa Mtwara kwa kipindi cha Miaka mitatu (3).

Tarehe 1/7/2001 alipandishwa cheo na kuwa Hakimu Mkazi Daraja la II.

Mnamo tarehe 25/2/2002 alihamishiwa Mkoa wa Iringa akitokea Mtwara kama Hakimu Mkazi wa Mkoa huo. Tarehe 27/10/2004 aliteuliwa kuwa Hakimu Mkazi daraja la I.

Tarehe 20/6/2006 aliteuliwa kuwa Msajili wa Wilaya Mahakama Kuu. Tarehe 14/11/2006 alipandishwa cheo na kuwa Hakimu Mkazi Mkuu daraja II.

Tarehe 9/5/2007 alihamishiwa Tabora kama Msajili wa Wilaya. Mnamo Tarehe 29/9/2009 aliteuliwa kuwa Hakimu Mkazi Mkuu daraja la I. Na mnamo tarehe 29/7/2010 alihamishiwa Mahakama kuu Kanda ya Dar es salaam akitokea Tabora.

Tarehe 15/7/2010 aliteuliwa kuwa Naibu Msajili Mwandamizi Mahakama Kuu ya Tanzania. Mnamo tarehe 15/6/2012 akiwa Naibu Msajili Mwandamizi aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania akapangiwa kuhudumu Divisheni ya Ardhi, baadaye tarehe 5/3/2013 alihamishiwa Masjala Kuu.

Tarehe 25/5/2016 aliteuliwa kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kanda ya Bukoba. Tarehe 10/7/2018 alihamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tabora akiwa ni Jaji Mfawidhi wa kanda hiyo hadi mauti yalipomfika tarehe 16/7/2020.

Mwili wa Marehemu Jaji Salvatory Bongele utazikwa nyumbani kwao Rombo, Kilimanjaro siku ya Jumanne Tarehe 21/72020.

BWANA AMETOA NA BWANA AMETWAA JINA LAKE LIHIMIDIWE.

 

 

Comments (0)

Leave a Comment