Post Details

UJENZI WA VITUO JUMUISHI VYA UTOAJI HAKI WASHIKA KASI NCHINI

Published By:LYDIA CHURI

Na Lydia Churi-Mahakama

Mahakama ya Tanzania inaendeleza kwa kasi ujenzi wa majengo ya vituo sita Jumuishi vya utoaji haki katika mikoa mitano nchini ikiwa ni hatua ya Mhimili huo ya kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

Ujenzi wa majengo hayo umeanza mwezi Januari mwaka huu na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Octoba mwaka huu.

Majengo ya Vituo Jumuishi vya utoaji haki yatakuwa na na sakafu nne yaani gorofa 3 na yatajumuisha ngazi zote za Mahakama kuanzia Mahakama Kuu mpaka Mahakama ya Mwanzo pamoja na ofisi za baadhi ya wadau wa Mahakama wakiwemo Polisi, Ustawi wa Jamii, Mawakili na Waendesha Mashitaka.

Majengo hayo yameanza kujengwa katika miji ya Arusha, Mwanza, Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam katika wilaya za Kinondoni pamoja na Temeke.

Kusudi la kuweka ngazi zote za Mahakama ndani ya jengo moja pamoja na ofisi za wadau ni kurahisisha mchakato wa upatikanaji wa haki pamoja na kumpunguzia mwananchi gharama.

Mahakama ya Tanzania inashirikiana na Benki ya Dunia katika ujenzi huo. Lengo la Mahakama ni kuwa na huduma ya Mahakama Kuu katika kila mkoa, Mahakama za Hakimu Mkazi katika kila Mkoa, Mahakama za Wilaya kwenye kila Wilaya na Mahakama za Mwanzo kwenye kila Tarafa kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha.

 

 

Comments (0)

Leave a Comment