Post Details

MAHAKAMA KUU KIGOMA YAVUKA LENGO KUSIKILIZA NA KUMALIZA MASHAURI

Published By:LYDIA CHURI

Na Lydia Churi-Mahakama, Kigoma

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma imefanikiwa kwa asilimia 100 kumaliza mashauri yote ya mlundikano na kuvuka kiwango kilichowekwa na Mahakama ya Tanzania.

Mahakama ya Tanzania ilijiwekea mkakati wa kumaliza mashauri ya mlundikano kwa kuweka muda wa shauri kumalizika mahakamani ambapo kwenye Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu shauri linatakiwa kumalizika katika kipindi cha miezi 24, Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za wilaya miezi 12 na Mahakama za Mwanzo ni miezi sita.

Akizungumza na Maafisa Habari wa Mahakama ya Tanzania, Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Kigoma Mhe. Ilvin Mugeta alisema kuanzishwa kwa Mahakama Kuu mkoani Kigoma na kujengwa kwa jengo jipya la Mahakama hiyo kumerahisisha shughuli za utoaji haki kwenye kanda hiyo ambapo hivi sasa hakuna mlundikano wa mashauri kwa viwango vilivyowekwa na Mahakama ya Tanzania. Aliongeza kuwa kwa upande wa Mahakama Kuu mashauri yalisikilizwa na kumalizika ndani ya miezi 24.

Jaji Mfawidhi huyo alisema licha ya Mahakama kuweka kiwango cha kitaifa, Kanda ya Kigoma pia ilijiwekea kiwango cha muda wa kumaliza mashauri ambapo kwa Mahakama Kuu ni miezi 6, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama za wilaya miezi minne wakati Mahakama za Mwanzo ni miezi mitatu.

 “Juni 30 mwaka huu tulifanya tathmini ya viwango tulivyojiwekea na kugundua kuwa tumefanikiwa kwa asilimia 77 kwani kati ya mashauri 115 yaliyokuwepo Mahakama Kuu, ni mashauri 19 tu ndiyo yalivuka miezi 6 nayo yalikuwa ni yale yaliyokatiwa rufaa na majalada yake yalikuwa yamecheleweshwa kutoka Mahakama za chini”, alisema Jaji Mugeta.

Kwa upande wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama za wilaya, Jaji Mfawidhi alisema baada ya tathmini ya Juni 30, hakukuwa na mashauri ya mlundikano kwa mashauri ambayo Mahakama hizo zina mamlaka nayo. “Tumefanikiwa kwa asilimia 71 kufikia lengo la kikanda la miezi 4 tulilojiwekea na lengo la kitaifa la miezi 12 pia tumefanikiwa kwa asilimia 100”, alisema.  

Kwa mujibu wa Jaji Mugeta, Kanda ya Kigoma imefanikiwa kwa asilimia 100 kuvuka lengo la kitaifa la kumaliza mashauri ndani ya miezi sita na lengo la Kanda la miezi mitatu iliyojiwekea kwa Mahakama za Mwanzo kwa kuwa mashauri yote 240 yaliyokuwepo kwenye Mahakama hizo yalisikilizwa na kumalizika katika kipindi cha miezi 3.

Kuhusu utoaji wa hukumu ndani ya siku 90, kanda ya Kigoma imefanikiwa kwani mpaka Juni 30 hakukuwa na shauri ambalo halikusomwa hukumu ndani ya siku 90 na pia kwa upande wa nakala za hukumu kanda hiyo ilifanikiwa kutoa nakala hizo ndani ya siku 21.

Aidha, Jaji Mugeta alisema kuhusu Mahabusu na Magereza, wamefanikiwa kusimamia mkakati wa taifa wa kuondoa msongamano wa mahabusu na wafungwa magerezani kwa asilimia 100. Tathmini iliyofanyika Juni 30 mwaka huu ilionesha kuwa hakukuwa na gereza lenye msongamano mkoani humo, magereza yote yalikuwa na idadi ya wafungwa na mahabusu kwa kadri ya uwezo wake.

Kuhusu matumizi ya Tehama kwenye kanda hiyo, Jaji Mfawidhi alisema vifaa vya Tehama vimefungwa kwenye Mahakama zote kuanzia Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama zote za wilaya. Aliongeza kuwa Magereza ya Kasulu, Kibondo na Bangwe tayari yamefungiwa vifaa hivyo isipokuwa magereza mawili ya Kwitanga na Ilagala ambayo yatafungiwa ifikapo Septemba mwaka huu.

Alisema mashauri 20 yanayohusu mahabusu yameshasikilizwa kwa njia ya Mahakama mtandao (Video conference) na mpango uliopo ni kuiwezesha ofisi ya Taifa ya Mashtaka kupata vifaa vya Tehama ili kurahisisha utendaji wa kazi.

Alisema Kanda ya kigoma inafanya vizuri kwenye matumizi ya mfumo wa kusajili mashauri kwa njia ya mtandao (JSDS ll) na imefikia hatua ya kuwasajili Mawakili wa kujitegemea kwenye mfumo huo kwa mujibu wa sheria ya kusajili mashauri kwa mtandao.

Mahakama ya Tanzania inaendelea na Maboresho ya huduma zake kwa kusogeza huduma zake karibu zaidi na wananchi kwa kujenga majengo mapya, kuboresha sheria na kanuni mbalimbali na kutumia Tehama kurahisisha shughuli za utoaji haki nchini.   

Comments (0)

Leave a Comment