Post Details

MAHAKAMA KUANZA UJENZI WA JENGO LA MAKAO MAKUU JIJINI DODOMA

Published By:LYDIA CHURI

Na Innocent Kansha- Mahakama

Mahakama ya Tanzania imesaini mkataba na Kampuni ya Reli kutoka nchini China CRJE (EAST AFRICA) kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama linalotarajiwa kuanza kujengwa hivi karibuni jijini Dodoma na kukamilika ndani ya miezi 24.

Hafla ya kutiliana saini kwa mkataba huo ilifanyika katika ofisi za makao makuu ya Mahakama zilizoko katika jengo la Mahakama ya Rufani Jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia mkataba huo,  Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru alisema anategemea muda waliokubaliana wa kupokea jengo hilo utakuwa ni kwa wakati muafaka na  litaendana na hadhi ya Muhimili husika.

‘‘Nategemea kuona tunapokea jengo zuri lenye ubora halisi unaoendana na thamani ya mkataba huu, kwani Mahakama ni moja ya nguzo ya Serikali hivyo hatutarajii kuona jengo lisilo lingana na hadhi ya Muhimili wenyewe,’ alisema Kabunduguru.

Aliongeza kuwa Mahakama ina wajibu wa kuhakikisha kila mtu anapata haki sio kwa Watanzania tu hata kwa wageni wanaofika hapa nchini kwa shughuli mbalimbali ikiwemo uwekezaji na Muhimili huo unatarajia kuwa na  jengo hilo liwe chachu ya uharakishaji wa utoaji haki kama ilivyo  katika jukumu  lake la msingi la kikatiba.

Mtendaji huyo aliitaka  ofisi ya Wakala wa Usimamizi wa Majengo Tanzania (TBA) itambue kwamba  inayo wajibu  wa kusimamia ujenzi huo sio kwa niaba ya Mahakama ya Tanzania bali kwa niaba ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwani Mahakama ni sehemu ya kiungo au Mhimili wa Serikali.

"Mkandarasi unayo kazi kubwa mbele yako ya kuhakikisha unatekeleza wajibu wako ipasavyo ili uweze kupimwa kwa thamani ya jengo hili.

‘‘Niwakumbushe tu kwamba leo hii tumeingia kwenye jukumu kubwa na zito la kutia saini ujenzi huu tunategemea kuona sio tu kazi iliyo bora bali kazi inayotazamwa na Taifa zima kwa ujumla, hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha ujenzi huu unafanikiwa kwa kiwango kinachokidhi hadhi ya Mahakama,’’ alisisitiza.

Naye Mwenyekiti wa Kampuni ya Reli ya Nchini china CRJE (East Africa) Bw. Xie Zhixiang alihihakikishia Mahakama kuwa kampuni yao ina uzoefu mkubwa katika kutekeleza miradi mikubwa ya aina hii, hivyo wanategemea kujenga kwa kiwango cha ubora wa hali ya juu kulingana na makubalianao ya ujenzi huo.

Kwa upande wa Mkandarasi Mshauri, Wakala wa Majengo Nchini (TBA), ambaye Msanifu wa Majengo Bw. Geofrey Munyaga alisema tunashukuru kwa kuaminiwa na serikali tupo tayari kutekeleza jukumu letu kikamilifu kama wasimamizi washauri katika mradi wa ujenzi huu tutahakikisha tunasimamia ubora wa ujenzi wa jengo hili unatekelezwa kama ilivyo kusudiwa na Serikali.

Ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania utakaoanza hivi karibuni jijini Dodoma unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miaka miwili kuanzia sasa.

Comments (0)

Leave a Comment