Post Details

SHERIA YA WANAWAKE NA WATOTO ZITAFSIRIWE ZIENDANE NA WAKATI

Published By:LYDIA CHURI

Na Tawani Salum – Mahakama

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Gerald Ndika amewashauri Majaji na Mahakimu kutafsiri sheria zinazohusu masuala ya wanawake na watoto ili ziendane na mazingira ya sasa katika kuendesha mashauri yanayohusu masuala ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia.

Akizungumza wakati wa Mafunzo ya Haki za Binadamu na Unyanyasaji hususan kwa  wanawake na watoto, yanayofanyika Bagamoyo Mkoani Pwani, Jaji Ndika alisema kuwa sheria zilizopo kwa kiwango kikubwa zinajitosheleza kinachotakiwa ni jinsi ya kuzitafsiri,  hivyo Majaji na Mahakimu watoe tafsiri ambayo inaendana na mazingira ya matukio yalivyo.

Jaji Ndika ambaye ni mshiriki katika mafunzo hayo,  alisema kuwa moja ya faida zake ni kuwaandaa wawezeshaji katika eneo hilo ili kusaidia Mahakama ya Tanzania, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mahakimu, na watumishi mbalimbali ambao wanatoa maamuzi juu ya  vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa wanawake na watoto kuwa na umahiri.

‘‘Matukio haya yanatokana na mambo mengi ikiwemo mila potofu pamoja na  uelewa mdogo, wanaona kumpiga mke au mtoto ni jambo la kawaida na ana haki ya kufanya hivyo. Lakini mafunzo haya yatasaidia kupata wakufunzi ambao wataenda kuwapa wengine elimu juu ya kuweza kupambana na ukatili na unyanyasaji wa wanawake na watoto,’’ alisisitiza Jaji Ndika.

Aliongeza kwamba mafunzo hayo,  ni ya mara ya tatu kufanyika yakiwa  ni endelevu katika kutoa elimu hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Joaquine De Mello akifungua rasmi mafunzo hayo, alisema kuwa  yana lengo la  kuwawezesha watoa maamuzi kuwa na uweledi zaidi  wa kutoa  haki na pia kuielimisha jamii  juu ya haki zao za msingi na tatizo la unyanyasaji na ukatili wa kijinsia ambalo limekithiri.

Aliongeza kwamba kumekuwa taarifa nyingi zinazotolewa na vyombo vya habari pamoja na wanajamii ambao wamejitokeza wazi kutoa matukio mbalimbali   juu ya suala hilo. Pia tafiti mbalimbali ambazo zimefanywa, hivyo wamegundua kuwa matukio mengi ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia yanafanywa wahusika  wanaotuhumiwa kuwa  ni familia au ndugu wa karibu.

Alisema kuna mapungufu katika jamii kama vile utamaduni wa kutokuwa na utayari wa kusimamia na kuyapigia kelele  tatizo hilo,  ikiwa  ni sababu mojawapo ya unyanyasaji na ukatili huo.

‘‘Kupitia mafunzo haya kama watoa maamuzi tunataka wapate jicho la kipekee shauri linapokuja mbele yako mara moja unapata picha kuwa hili ni la kikatili na unalipa nafasi yake na hii itasaidia katika kuandaa taarifa ya matukio haya kwa usahihi, ikiwemo kuwa na  takwimu ambazo tunazihitaji ili kujua nguiu gani ya ziada inahitajika katika kusimamia jambo hili,’’ alisema Jaji De Mello.

Mshiriki mwingine wa mafunzo hayo, ambaye ni Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine, Mhe,  Hanifa Mwingira alisema jamii inapaswa kuona kuwa vitendo hivyo ni vibaya na kila mtu anapaswa kusema ‘ukatili sasa basi na mtoto wa mwenzako kuwa ni mtoto wako na hupaswi kumfanyia ukatili,’.

Mwingira alifafanua kuwa mafunzo hayo yametolewa kwa viongozi wa dini ambao watawaelimisha  waumini wao, wakiwemo  Wenyeviti wa vijiji, kata pamoja na mitaa na Maafisa wa Ustawi wa Jamii, Polisi, Magereza na wadau wengine wa  sheria.

Mafunzo hayo yanayoendelea yanahudhuriwa na Majaji Wastaafu akiwemo Jaji  Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Salum Massati ambaye anashiriki kama mtoa mada,

Jumla ya washiriki 26 wanapatiwa  mafunzo hayo yaliyoanza Juni 27, mwaka huu na yatamalizika Julai Mosi.

Comments (0)

Leave a Comment