Post Details

KAMATI YAASWA KUONGEZA TIJA KATIKA MABORESHO YA MAHAKAMA

Published By:LYDIA CHURI

Na Magreth Kinabo- Mahakama

Kamati  mpya ya Mafunzo na Utafiti ya Jaji Mkuu wa Tanzania, leo imeanza kikao chake cha nne cha mwaka wa fedha wa 2019/2020 na kujadili majukumu mbalimbali ya kamati hiyo.

Akifungua  kikao hicho cha siku mbili, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe.  Bethuel Mmilla alisema  wana jukumu la  kuongeza ushirikiano wa kuendelea kuleta mageuzi  katika maboresho yanayofanywa na Mahakama ya Tanzania.

Kikao hicho kinafanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi, iliyopo Jijini Dar es Salaam.

‘‘Dhumuni kuu, la kuwa na kamati hii ni kuongeza ushiriki mpana ili mageuzi haya tunayosimamia wenyewe yapate ushiriki wenu wa karibu zaidi na michango bora, muhimu na itakayoleta ufanisi na tija kwenye Taasisi hii muhimu ya uendeshaji wa nchi yetu,’’ alisema Jaji Mmilla.

Jaji Mmilla  aliyataja baadhi ya majukumu ya kamati hiyo, kuwa ni kufanya kazi kwa karibu na Idara ya Mafunzo, Idara ya Utafiti, Ufuatiliaji na Tathmini na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa  Mahakama Lushoto (IJA), kupitia Idara ya Mafunzo endelevu iliyopo chuoni hapo kama kiungo, kupendekeza Sera ya Mafunzo endelevu ya Maafisa wa Mahakama na wengine.

Majukumu mengine ni kushauri  Baraza la Chuo cha Uongozi wa  Mahakama Lushoto (IJA) moja kwa moja ama kupitia kupitia Mwenyekiti wa Baraza la Chuo au wajumbe  toka Mahakama, kuendekeza aina mbalimbali za mafunzo endelevu, kumshauri Mkuu wa chuo cha IJA juu ya mahitaji na vipaumbele vya Mahakama juu ya mafunzo endelevu.

Aidha aliongeza kwamba kamati hiyo itakuwa na kazi ya kufanya utambuzi na kuwa na orodha ya Wakufunzi na vyuo kwa ajili ya mafunzo endelevu kwa viongozi na watumishi wote kulingana na mahitaji na kufuatilia, kuchambua na kutathmini mafunzo mafunzo endelevu na mengine ya Maafisa wa Mahakama wakiwemo wengine.

Kamati hiyo ina wajumbe saba, ambayo Jaji Mmilla, Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Augustine Mwarija na Mhe. Winifrida Korosso, wengine ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Lameck Mlacha, na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.Dkt. Benhaji Masoud na Mhe. Dkt. Modesta Opiyo, akiwemo Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe  Dkt. Paul Kihwelo, ambaye ni Mkuu wa chuo cha IJA.

Wajumbe hao waliteuliwa rasmi na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma Aprili 8, mwaka huu na watadumu katika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu.

Kamati zingine zilizoundwa na Jaji Mkuu ni Kamati ya Kanuni, Kamati ya Takwimu na TEHAMA, Kamati ya  Ufuatiliaji na Tathmini na Kamati ya Maboresho.  

 

 

Comments (0)

Leave a Comment