Post Details

MABORESHO YA KANUNI YANAVYORAHISISHA UPATIKANAJI HAKI

Published By:LYDIA CHURI

Na Innocent Kansha - Mahakama

Mahakama ya Tanzania imefanya Maboresho na inaendelea kufanya maboresho katika maeneo yote muhimu ya utendaji kazi kupita nguzo tatu za Mpango Mkakati wa Miaka Mitano ulioanza kutekelezwa mwaka 2015/16 hadi mwaka 2019/20.

Nguzo hizo ni Utawala, Uwajibikaji na Matumizi ya Bora ya Rasilimali, Upatikanaji wa haki sawa  kwa wote na kwa wakati na Kujenga taswira chanya na Kurejesha imani ya wananchi kwa Mahakama.

Hivyo maboresho ya sheria na kanuni mbalimbali yaliyofanywa na Mahakama ya Tanzania katika kurahisisha utoaji wa haki maana yake ni kuhakikisha sheria zile ambazo hazikuwa rafiki  zilikuwa na muonekano wa utaratibu wa zamani basi kuwekewa utaratibu mpya unaoendana na hali ya sasa

Kwa upande wa kanuni kama zilikuwa na utaratibu ambao sasa umepitwa na wakati basi kupitia Maktaba Kuu  ya Mahakama ya Tanzania, hupokea majuzuu ya sheria hizo kwa kushirikiana na Katibu wa Kamati ya Sheria/Kanuni,  ambayo huweza kushauri sheria zipi na kanuni zipi ambazo ni za zamani zinazohitaji kuboreshwa

Maboresho yanafanyika pale ambapo  kamati  hiyo inaona kwamba sheria za  sasa, katika muda huu hazifai kutumika na  ni vitu gani vinafaa kutumika.

Akizungumzia kuhusu maboresho hayo,  Kaimu Mkuu wa  Kitengo cha Maktaba Mahakama ya Tanzania Mhe. Kifungo Mrisho , ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo  alisema ‘‘Katibu wa Kamati ya Sheria na  Kanuni huchukua kile ambacho huonekana ni bora na kuhakikisha kwamba kanuni/sheria hizo zinafika kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni/Sheria.  Mwenyekiti huyo  huchaguliwa na Jaji Mkuu akipata mawazo yoyote kuhusu maboresho ya sheria/kanuni huwasiliana na Jaji Mkuu ili kuitisha kamati  kupitia sheria hizo na kuweka maboresho hayo kama ni ya sheria au kanuni”.

Kamati hiyo inakuwa na utaratibu wa kuchukua maoni hayo ambayo yamekamilika na sheria hizo ambazo zimefanyiwa mabadiliko na kuwasilisha kwa Jaji Mkuu, ambaye ana uwezo wa kuhakikisha kwamba sheria na kanuni hizo ambazo zimefanyiwa marekebisho zinapelekwa kwa wadau, ambao ni wahe. Majaji, Wasajili, Mahakimu na Mawakili wa kujitegemea kwa ajili ya kuleta maoni yao.

Mrisho aliongeza maoni hayo yakishaletwa kamati hiyo hukaa vikao kwa ajili ya kuyaangalia na kuweza kutunga sheria/kanuni iliyokamili ili kuja na sheria/kanuni iliyokamili kwa ajili ya kuhakikisha kwamba maboresho yamefanyika kuendana na wakati.

‘‘Kwa kifupi tu, ni  kwamba Mhe. Jaji Mkuu kupitia Sheria Sura Namba 354 Judicature and Application of laws Act (JALA) sheria hii humpa mamlaka ya kutengeneza kanuni za Mahakama Kuu, lakini pia katika sheria yoyote ile inayotungwa na Bunge,  hata hivyo kuna zinazompa mamlaka Waziri kutengeneza kanuni au taratibu za kimuongozo wa namna gani sheria husika itumike lakini kuna sheria zingine zinazompa mamlaka Jaji Mkuu kutengeneza kanuni au taratibu .

Akitolea ufafanuzi wa taratibu za maboresho alisema pale ambapo Jaji Mkuu amepewa mamlaka ya kutengeneza sheria fulani au kanuni kupitia kamati yake ikishaona hilo, kwa mfano, Sheria ya Vyombo vya Habari iliyotungwa mwaka 2017 (Media Service Act of 2017) Mhe. Jaji Mkuu alipaswa kutengeneza kanuni. ‘‘Hivyo kamati hiI hungalia zile sheria zinazotakiwa kutungiwa kanuni na kumshauri , Jaji Mkuu ambaye hutoa agizo kwa kamati sasa kanuni zitengenezwe”.alisisitiza.

Alisema  hata kama kuna sheria yoyote ya mabadiliko inayohitaji maboresho yanayofanyika bungeni au labda inataka kwenda bungeni bado kamati hiyo hushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikisha kwamba ile sheria ambayo inakuja basi iwe na ahuweni katika ubora kwa ajili ya kuendeshwa katika Mahakama na misingi mizuri ya upatikanaji wa haki.

“Hata mwaka 2016 kamati ya kanuni iliweza kupendekeza mabadiliko ya Sheria Sura Namba 141 ambayo ni Sheria ya Rufani inayotoa mamlaka ya kusajili rufaa katika Mahakama ya Rufani Tanzania haikuwa na kipengele cha mapitio (review) lakini kamati ya kanuni iliweza kushauri kufanyika maboresho hayo” alisema Mrisho.

Mabadiliko ya Kanuni za Mahakama ya Rufani Tanzania ya  2019  (The Tanzania Court of Appeal Rules) yameleta kanuni za utendaji haki, bila kuzingatia taratibu za kiufundi zilizopitiliza (overriding objectives).

Kanuni hizi zinajulikana Kama “oxygen principle” Kama zinavyoainishwa chini ya kifungu cha 3A na 3B cha Sheria ya Mamlaka ya Mahakama ya Rufani Tanzania (The Appellate Jurisdiction Act). Kanuni hizi zinaitaka Mahakama kuepuka taratibu za kiufundi katika kufikia utoaji wa haki.

Kuanzia mwaka 2016, 2017, 2018 na 2019 kuna mabadiliko ya maboresho ya kanuni mengi yamekwishafanyika na yapo kwenye matumizi lakini ni mabadiliko yanayoletwa na maboresho ya sheria zinazotumika mahakamani kwa kupitia kamati hiyo.

Alifafanua kuwa hadi  sasa sheria na kanuni , ambazo zimekwisha pitishwa na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali ni kanuni 41,  lakini mapendekezo mengi yamekwisha fanyiwa kazi na kamati ya maboresho, pia takribani sheria 38 zimefanyiwa kazi ingawa hazitangazwa katika gazeti hilo.

Lengo likiwa ni kurahisiha utaratibu mzima wa uendeshaji wa mashauri kuanzia hatua ya awali ya upokelewaji wa shauri hadi hatua ya mwisho kabisa ya utekelezaji wa tuzo uliotokana na hukumu au uamuzi ama amri ya Mahakama.

Mrisho  alisema kuwa  ikumbukwe kamati hiyo  ilianzishwa Julai, mwaka 2014 wakati wa utawala wa Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu Othuman Chande na Mwenyekiti   wake wa kwanza alikuwa Mhe. Jaji Edward Rutakangwa kamati inaundwa na Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani   Tanzania wanne, Wahe. Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wanne na pia sekretarieti ya wataalamu watatu   ambao wote ni wanasheria wabobezi.

Hadi mwaka 2019 wakati kamati   hiyo ilifanya kazi ya mwisho ya kupitisha utaratibu wa kuweza kutoa hukumu au kutoa adhabu kwa mahakimu (Sentencing Guideline Manual) ambao umepitishwa Desemba, mwaka 2019, na Kamati ya Maboresho ya Kanuni na kuzinduliwa. Januari 31, mwaka 2020.

Hizi zote ni taratibu ambazo zinazoboresha ufanisi wa kazi wa Mahakama, utaratibu huu umewekwa kisheria ufuatwe ili kuongeza tija katika utendaji wa kazi.

“Kamati hii inashughulikia mambo mengi kama vile kutoa mapendekezo juu ya utoaji wa vitabu mbalimbali vya maelekezo au miongozo mfano kamati inatoa ushauri juu utoaji wa kitabu cha maelekezo au mwongozo wa ukazaji wa hukumu (Execution Guideline Manual), pia kuna mwongozo mwingine wa watumiaji wa Mahakama ili kuwapa uelewa mpana watumiaji kujua taratibu za Mahakama.(Court users Guideline Manual)” alisema.

Kingine cha Mwongozo wa Usimamizi wa Mashauri (Case Management Guideline) hii inasaidia taratibu za uendeshaji wa kesi mahakamani, kitaelezea taratibu za uendeshaji wa kesi mbalimbali kama vile madai, jinai, talaka, mirathi na kesi nyingine nyingi zinazofunguliwa mahakamani.

Kwa upande wake Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.Shamillah Sarwatt, alisema maboresho haya yametoa mwanga chanya kwa Mahakama na wadau mfano; Kanuni za Kusajili kesi kwa njia ya Mtandao (Electronic Filing Rules) za mwaka 2018.

‘‘Zinatoa fursa kwa Wakili wa Serikali na wa kujitegemea ama mtu mwingine yeyote kusajili shauri mahala popote pale alipo bila kulazimika kufika mahakamani kwa kutumia Teknologia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), vivyo hivyo kwa kutumia kanuni hizi mlolongo wa taratibu nzima za usajili wa mashauri umerahisishwa na hivi sasa inachukua siku moja tu badala ya hapo awali ilikuwa inachukua muda mrefu zaidi,”alisema. Msajili huyo.

 Sarwatt  aliongeza kuwa mabadiliko mengine  yaliyofanyika  ni  ya Sheria Anuai Namba 8 ya Mwaka 2018 ambayo imefanyiwa marekebisho,  ikiwemo Sheria ya Mamlaka ya Mahakama ya Rufani  Tanzania, iliyoiwezesha Mahakama hiyo,  kutofungwa na sababu za kiufundi wakati wa kusikiliza shauri.

Nyingine ni Sheria ya Migogoro ya Ardhi Sura Namba 216 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002 (Land Dispute Act Cap. 216 RE 2002) nayo imefanyiwa marekebisho na kuruhusu Wahe. Mahakimu wenye mamlaka ya nyongeza kusikiliza mashauri ya migogoro ya ardhi katika Mahakama Kuu  ya Tanzania.

Kupitia maboresho kuna mabadiliko ya jedwali la sheria za madai na taratibu zake ya mwaka 2019, yamepunguza hatua za usikilizwaji wa mashauri ya madai kutoka hatua 38 hadi hatua 22 tu zitakazo tumika mahakamani.

Maboresho haya lengo lake ni kusaidia uharakishwaji wa utoaji wa haki kwa wakati na kwa wote, urahisishaji wa utaratibu mzima wa kuendesha mashauri unalenga katika kupunguza muda wa shauri kukaa mahakamani hivyo kutoa fursa kwa mdaawa wa shauri kutumia muda huo katika shughuli za uzalishaji mali kwa faida ya mtu mmoja mmoja na kwa Taifa letu kwa ujumla.

Comments (0)

Leave a Comment