Post Details

JAJI KIONGOZI ATEMBELEA GEREZA KUU ISANGA DODOMA

Published By:faustine.kapama

Na Arapha Rusheke-Mahakama, Dodoma.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, jana tarehe 20 Machi, 2023 alifanya ziara ya kikazi ya Mahakama katika Gereza Kuu Isanga jijini hapa kukagua shughuli na maeneo mbalimbali.          

Hii ni mara yake ya kwanza kufanya ziara hiyo tangu ateuliwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo tarehe 8 Oktoba, 2021, kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na mtangulizi wake, Mhe. Dkt. Jaji Eliezer Feleshi aliyeteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mhe. Siyani alipokelewa na Mkuu wa Magereza ya Mkoa wa Dodoma, Bi. Bertha Minde aliyeambatana na mwenyeji ambaye ni Mkuu wa Gereza la Isanga. Akiwa katika ofisi ya Mkuu wa Gereza hilo, Jaji Kiongozi alipokea taarifa ya magereza yote ya Mkoa wa Dodoma na baadae kupewa taarifa fupi ya Gereza Kuu Isanga.

Baada ya hapo, Mhe. Siyani alikagua maeneo mbalimbali ya Gereza, ikiwemo vyumba wanavyolala wafungwa, Zahanati ya ndani ya gereza, jikoni kunakopikwa chakula na akamalizia ukaguzi wake kwenye kiwanda cha kufuma vikapu vinavyotokana na mkonge.

Baadaye aliwatembelea kwa nyakati tofauti tofauti mahabusu na wafungwa wa kiume na wa kike wa makosa ya kawaida pamoja na wale waliohukumiwa kunyongwa na kufanya nao baraza.

Katika matukio hayo, Jaji Kiongozi alipokea risala zao na kusikiliza hoja mbalimbali, changamoto na maswali ambayo baadhi aliyajibu na kutoa maelezo mafupi.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mhe. Siyani alieleza kuwa haki ya wafungwa na mahabusu haikamilishwi na taasisi moja, hivyo kila moja inatakiwa kufanya shehemu yake ili kuhakikisha wanapata haki zao kwa wakati.

Jaji Kiongozi aliwapa pole kwa kuwa hakuna mtu anayependa kukaa gerezani na kuwasihi wale watakao bahatika kutoka kwa namna yeyote ile kutofanya mambo ambayo yatawarudisha tena huko.

Katika ziara hiyo, Jaji Kiongozi aliambatana na viongozi wa Mahakama ya Tanzania kutoka Makao Makuu, wakiwemo Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe Wilbert Chuma, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Shamillah Sarwatt, Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Mhe Dkt. Adam Mambi, Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Bw. Sumera Manoti pamoja na viongozi wengine.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam).

Comments (0)

Leave a Comment