Post Details

MASHAURI 4,711 YASIKILIZWA KWA MTANDAO NDANI YA MIEZI MIWILI

Published By:LYDIA CHURI

Na Magreth Kinabo

Mahakama ya Tanzania imefanikiwa kuendesha mashauri 4,711 kwa njia ya Mahakama Mtandao maarufu kama ‘Video Conference’ katika kipindi cha miezi miwili ikiwa ni hatua mojawapo  ya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID 19.

Mashauri  hayo yamesikilizwa kwa njia  hiyo, kufuatia  utekelezaji wa agizo la Jaji Mkuu wa  Tanzania, Prof. Ibrahim  Hamis Juma alilolitoa Machi 23, mwaka huu la matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuwaepusha Watumishi wa Mahakama pamoja na wadau wake dhidi ya maambukizi hayo, wakati shughuli za utoaji haki zikiendelea kufanyika. 

Akizungumzia usikilizaji wa mashauri kwa kutumia teknolojia hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Mahakama ya Tanzania Bw. Machumu Essaba alisema hatua hiyo imelipunguzia Jeshi  la Magereza gharama za usafiri wa kila siku za kuwaleta wafungwa au mahabusu mahakamani na pia kupunguza msongamano.

“Njia hii imetumika katika kipindi cha ugonjwa huu, kuanzia Machi 23, mwaka huu  hadi Mei 26, mwaka huu, ambapo Mahakama ya Rufani ya Tanzania, imesikiliza mashauri 48 kupitia vikao vitano, kati ya hivyo vitatu vilifanyika katika Jiji la Dar es Salaam, vilivyohusisha mashauri 30 na kimoja Tabora kilichohusisha mashauri tisa, wakati mashauri tisa yalisikilizwa katika kikao kilichofanyika kanda ya Iringa” alisema Essaba.

Alisema  Mahakama Kuu ya Tanzania  Kanda ya Dar es Salaam imesikiliza mashauri 3,188 kati ya hayo, mashauri 804 yamesikilizwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mahakama za Wilaya, Kinondoni 714, Ilala 992, Temeke 523, na  Kigamboni 155.

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya, Mahakama ya Mkoa na Wilaya mashauri yaliyosikilizwa kwa teknolojia hiyo ni 367,  kanda  nyingine ni Tanga (310), Musoma (158), Tabora (130), Dodoma (78), Mtwara (66), Moshi (46), Arusha (41), Kigoma, (37),  Sumbawanga (23),  Iringa (15), Songea (14), Shinyanga (12), Mwanza (28) na Bukoba (5).

Essaba  alifafanua kwamba Mahakama Kuu Divisheni za Biashara imesikiliza mashauri 55 na Divisheni ya Kazi mashauri 90, ambazo zilitumia vifaa vilivyopo kwenye maeneo yao.

Aidha  aliongeza kwamba  zaidi ya mashauri 300 yamesikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza kwa kutumia simu ya mezani ‘Teleconference’ kwa sababu kuna tatizo la ukosefu wa huduma ya  mtandao ‘internet’ kwenye ofisi  za Mwanasheria  Mkuu wa Serikali, hali inayosababisha kutumia njia hiyo. 

Uongozi wa Mahakama katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kukabiliana na Virusi vya Corona ulikabidhi vifaa vya TEHAMA kwa Maafisa TEHAMA wa kanda 16 za Mahakama Kuu ya Tanzania Aprili 16 mwaka huu ili kuziwezesha Mahakama nyingine kusikiliza mashauri kwa  teknolojia hiyo.

Awali teknolojia hiyo ilikuwa inatumika katika vituo sita, ambavyo mfumo huo, umefungwa. Vituo hivyo ni Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda za Dar es salaam, Mbeya, na Bukoba pamoja na Kituo cha Mafunzo cha Kisutu, Gereza la Keko na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), Lushoto. 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Comments (0)

Leave a Comment