Post Details

KAMATI YA BUNGE KATIBA NA SHERIA YAIMWAGIA SIFA MAHAKAMA UBORESHAJI MIUNDOMBINU

Published By:Mary C. Gwera

-Yashauri huduma zitolewazo ziendane na uzuri wa majengo

Na Tiganya Vincent, Mahakama -Tabora

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria leo tarehe 14 Machi, 2023 imekagua Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora ambapo wameonesha kuridhishwa kwa kazi iliyofanyika na kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa utekelezaji mzuri wa Miradi mbalimbali ya uboreshaji wa miundombinu ya majengo yake.

Akizungumza mara baada ya ziara ya siku moja ya ukaguzi wa Utekelezaji wa Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe.  Florent Laurent Kyombo amesema kuwa Mahakama ni moja ya Taasisi inayofanya vizuri katika miradi yake ya ujenzi na hivyo kuwasihi Watumishi wa Mhimili huo kutoa huduma zinazoendana na uzuri wa miundombinu hiyo.

"Kama Kamati tuna 'oversee' mambo mbalimbali yanayofanyika Serikalini, hivyo napenda kuchukua nafasi hii kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa uboreshaji wa huduma mbalimbali unaoendelea ikiwa ni pamoja na maboresho ya miundombinu ya majengo, kwakweli mnaupiga mwingi," amesema Mhe. Kyombo.

Mhe. Kyombo ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa Mahakama ya Tanzania kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya utoaji haki kwa wananchi.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Kiteto ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati hiyo,  Mhe. Edward Ole Lekaita amesema ubora wa majengo ya Mahakama unaridhisha na kuongeza Mahakama imeitendea haki fedha waliyopewa na Serikali kwa ajili ya shughuli hiyo ya ukarabati.

Amesema uboreshaji na ukarabati wa Mahakama hiyo umewawezesha Maafisa wa Mahakama na Wadau wao kutekeleza majukumu yao ya utoaji wa haki kwa wananchi katika mazingira mazuri.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Khadija Shaaban almaarufu Keysha amesema Mahakama imeitendea haki fedha za ukarabati walizopatiwa na Serikali na kushauri kuweka 'Lift' maalum kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum.

Awali, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema Mradi huo umetumia kiasi cha fedha za Kitanzania bilioni 2.5 na ulianza kutekelezwa mwezi Juni mwaka 2021 na kukamilika Septemba, 2022.

Amesema kuwa, hadi sasa Mkandarasi ameshalipwa kiasi cha shilingi bilioni 1.5 ambayo ni sawa ya asilimia 61 na bado anadai milioni 900 ambazo wanaendelea kushughulikia.

Prof. Ole Gabriel, ameongeza kuwa, kukamilika kwa mradi huo kumesaidia kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora na kuahidi kuwa watahakikisha kuwa haki inapatikana kwa ubora.

Aidha Mtendaji huyo amewataka Wajumbe wa Kamati hiyo kuisaidia Mahakama kwa kuwaeleza wananchi kuhusu uboreshaji wa huduma mbalimbali za Mahakama unaoendelea ikiwemo matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wakati ufunguaji wa mashauri na usikilizaji wa mashauri.

Kamati hiyo inatarajia pia kutembelea jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC)-Mwanza tarehe 16 Machi, 2023.

Comments (0)

Leave a Comment