Post Details

WATOTO WASITUMIKE KUTOA USHAHIDI WA UONGO MAHAKAMANI: JAJI NGWEMBE

Published By:faustine.kapama

  • Aonyesha kukerwa na porojo za mapenzi ya jinsia moja

Na. Evelina Odemba – Mahakama Morogoro 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe amekemea tabia ya baadhi ya wazazi na walezi wanaowatumia watoto kutoa ushahidi wa uongo mahakamani. 

Mhe. Ngwembe alitoa rai hiyo hivi karibuni wakati akitoa elimu ya msingi ya sheria kwa wananchi waliofika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro kwa ajili ya masuala mbalimbali, ikiwemo kupata elimu hiyo. 

Alisema katika jumuiko la utoaji wa elimu hiyo lililoanza tarehe 7, Machi 2023 na kuhitimishwa leo tarehe 9, Machi 2023, kuwa kitendo cha kupeleka ushahidi wa uongo kimekuwa kikipelekea watuhumiwa kutumikia adhabu ya muda mrefu, ikiwemo kifungo cha maisha gerezani, bila kuwa na hatia. 

“Tunawaomba wananchi kujiepusha na vitendi hivi kwani ikibainiska sheria zipo wazi kwa mtu anayetoa ushahidi wa uongo mahakamani na hatua zitachukuliwa dhidi yake,” Jaji Mfawidhi huyo alisema.

Alitolea mifano ya baadhi ya kesi zilizokatiwa rufaa baada ya watuhumiwa kupewa adhabu ya kutumikia miaka 30 gerezani baada ya watoto kutumika kutoa ushahidi. 

“Lakini uchunguzi ulipofanyika upya ikagundulika kuwa watuhumiwa wale hawakutenda kosa hilo, isipokuwa walitiwa hatiani kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani baada ya mtoto kufundishwa kusema uongo,” alisema. 

Sambamba na hilo, Mhe. Ngwembe alizungumzia mmomonyoko wa maadili katika jamii, ikiwemo mapenzi ya jinsia moja na kuwaasa wananchi kuvikataa na kuvikemea kwa nguvu zote vitendo hivyo. 

Aliongeza kuwa vitendo hivyo hupelekea kuwepo kwa kesi nyingi za ulawati kwa watoto wadogo, hivyo ni jukumu la kila mmoja anaposhuhudia vitendo hivyo kutoa taarifa kwenye vyombo husika ili hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika. 

“Sisi wasomi tusiipotoshe jamii kuwa hili linaruhusiwa kisheria, kanuni ya adhabu kifungu cha 154 kinatamka wazi kuwa kosa hili la mapenzi ya jinsia moja adhabu yake ni kifungo kisichopungua miaka 30 gerezani,” alisisitiza. 

Katika jumuiko hilo, Jaji Mfawidhi huyo pia alifundisha masuala mbalimbali ya ulinzi wa mtoto, maadili katika jamii na malezi ya mtoto. Kadhalika, alifundisha kuhusu jamii kumlinda mtoto kuanzia akiwa tumboni mwa mama yake. 

Naye Mwananchi Jane Smart aliishukuru Mahakama kwa kuanzisha darasa la elimu ya msingi ya sheria kwakuwa wanapata mambo mengi ya msingi. Ameahidi kuwa barozi mzuri wa kukemea ukatili kwa watoto. 

Mahakama Kanda ya Morogoro ilizindua rasmi utoaji wa elimu ya sheria kwa wananchi awamu ya pili mnamo tarehe 2 March, 2023 baada ya awamu ya kwanza kuisha kwa mafanikio ya kuwafikia wananchi zaidi ya laki mbili. 

Mpango huu wa kutoa elimu ya sheria awamu ya pili unatarajiwa kufanyika ndani ya kipindi cha mwaka mzima wa 2023, ambapo mada mbalimbali zitafundishwa na wataalamu wa sheria kwa kusaidiana na wadau wa Mahakama na Haki Jinai.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Morogoro).

Comments (0)

Leave a Comment