Post Details

MWILI WA JAJI RAMADHANI WAZIKWA JIJINI DAR ES SALAAM

Published By:LYDIA CHURI

Lydia Churi- Mahakama

Mwili wa aliyekuwa Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Augustino Ramadhani umezikwa leo katika makaburi ya familia yaliyopo Kimara King’ong’o baada ya ibada ya kumuaga iliyofanyika katika kanisa la Anglikana la Mt. Albano jijini Dar es salaam.

Ibada hiyo iliyoongozwa na Askofu wa Kanisa hilo Mhe. Sosthenes ilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi pamoja na Viongozi mbalimbali kutoka Taasisi za Serikali, Mahakama na Taasisi za Kidini.  

Akimuelezea Marehemu Jaji Augustino Ramadhani, Prof. Kabudi alisema alikuwa ni aliyefanya mageuzi makubwa na maendeleo ya Zanzibar. “huwezi kuzungumzia mageuzi na maendeleo ya Zanzibar bila ya kumtaja Jaji Ramadhani”, Tanzania imepoteza mtu muhimu, hodari, muadilifu na mchapakazi”,alisema.

Aidha, mwili wa Jaji Mkuu Mstaafu huyo ulizikwa kwa heshima zote za kijeshi kwa kupigiwa mizinga 21 kama ishara ya kutoa heshima za mwisho kwa Brigedia wao  taratibu za kijeshi.

Wakati huo huo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limemuelezea Brigedia Generali Augustino Ramadhani kuwa ni mtu makini, muadilifu na mchapakazi na kuwa jeshi hilo limempoteza mshauri na mwalimu wa masuala ya kijeshi.

Akitoa salaam za jeshi hilo kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi, Generali Venance Mabeyo, Meja Generali Othman alisema Mkuu wa Majeshi amepokea taarifa za msiba huo kwa masikitiko makubwa na kwa niaba ya jeshi hilo anatoa pole kwa familia kutokana na kumpoteza mpendwa wao.

Naye mtoto wa marehemu Bw. Francis Ramadhani aliishukuru Serikali, Mahakama ya Tanzania, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Waumini wa kanisa la Anglikana pamoja na wananchi wote kwa ujumla kwa kuonyesha mshakamano mkubwa katika msiba wa baba yao.

Jaji Ramadhani alifariki dunia Aprili 28, mwaka huu saa 1:00 asubuhi katika Hospitali ya Agha Khan jijini Dar es salaam, baada ya kuugua kwa muda mrefu maradhi ya saratani  na mwishoni kupata Mshtuko wa Moyo (Heart Attack).

Marehemu Jaji Ramadhani alianza kuugua mwaka 2010 na kugundulika kuwa na ugonjwa wa saratani ambapo alitibiwa katika hospitali mbalimbali nje na ndani ya nchi. Hospitali alizotibiwa ni pamoja na hospitali za Apollo na Bangalore nchini India, Afrika ya Kusini, Nairobi Agha Khan na Dar es salaam Agha Khan. 

Comments (0)

Leave a Comment