Post Details

MAREHEMU JAJI RAMADHANI KIONGOZI MAHIRI NA MUADILIFU

Published By:LYDIA CHURI

Na Lydia Churi -Mahakama

Mwili wa aliyekuwa Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Augustino Ramadhani umeagwa rasmi leo katika viwanja vya Karimjee huku akielezewa kuwa alikuwa ni Kiongozi mahiri na muadilifu aliyeitumikia Mahakama ya Rufani kwa zaidi ya miaka 21.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema Marehemu Jaji Ramadhani ameacha hazina kubwa ya maarifa, uzoefu na maono ambayo ni jukumu la watanzania kukusanya, kuelewa na kujifunza.

Alisema Jaji Ramadhani alidumu katika Mahakama ya Rufani kwa takriban miaka 21, kuanzia alipoteuliwa na Mhe. Rais Ali Hassan Mwinyi mwaka 1989 kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, hadi tarehe 27 Disemba 2010, alipostaafu akiwa Jaji Mkuu.

“Miaka hiyo 21 ilikuwa ni miaka ya kutoa maamuzi ya mwisho ya kimahakama yenye nguvu kubwa ya kisheria. Kupitia maamuzi hayo, sauti yake ya kimaamuzi itaendelea kutuongoza kwa muda mrefu”, alisema Jaji Mkuu.

Prof. Juma alisema kuwa ni Majaji wachache wanajaaliwa kupata nafasi ya kutoa huduma za utoaji haki katika Mahakama zilizo juu kwa kipindi kirefu, hivyo kutokana na uzoefu wake, jambo lolote alilokuwa akilisema au kuliandikia, lilikuwa limebeba uzoefu na kuboreshwa hasa kwa kuwa alifanya kazi sehemu mbali mbali.  

Akimuelezea marehemu Jaji Ramadhani, Jaji Mkuu alisema alikuwa ni mtu   aliyependa maboresho ya Mahakama na Sekta ya Sheria kwa kushiriki katika mageuzi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushiriki katika hatua za mwanzo wakati Rasimu ya Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama (Judiciary Administration Act, 2011) ilipokuwa ikitayarishwa kabla ya kuwasilishwa Bungeni.

Alisema marehemu Jaji Ramadhani alipenda kutumia hukumu zake kama njia ya kuelimisha, kufafanua na kupendekeza maboresho. Aliongeza kuwa katika miaka yake ya utumishi mahakamani alishiriki katika kuamua mashauri mengi ambayo yalisheheni elimu, tafsiri na hata mapendekezo ya mabadiliko ya sheria huku akiwahimiza Mawakili wa Serikali, na wananchi kwa ujumla kuwa na utamaduni wa kusoma hukumu mbali mbali zinazotolewa Mahakama.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, Mahakama itafanya kumbukumbu rasmi ya kumuaga Marehemu Jaji Ramadhani Kitaaluma Mwenyezi Mungu atakapojaalia janga la COVID 19 kuisha.

Akitoa shukrani kwa Serikali, Jaji Mkuu amemshukuru Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa ukaribu aliouonyesha kwa Marehemu, tangu alipokuwa akimtembelea alipolazwa Hospitali ya Aga Khan kumjulia hali. Jaji Mkuu pia amemshukuru Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, kwa kufanikisha shughuli ya leo kupitia Kamati ya Kitaifa ya Mazishi ya Viongozi wa Kitaifa ambayo yeye ni Mwenyekiti kwa mujibu wa Sheria inayoratibu Mazishi ya Viongozi wa Kitaifa ya 2006.

Aidha amesema amepokea salaam za pole kwa Mahakama ya Tanzania na kwa familia kutoka kwa Majaji wakuu wa Uganda, Kenya, Rwanda, Gambia pamoja na Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki Prof. Emmanuel Ugisherabuka. Wote wakielezea namna walivyomfahamu na kumheshimu Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani.

Viongozi mbalimbali wa Kitaifa walishiriki kuaga mwili wa marehemu Jaji Ramadhani wakiwemo Marais Wastaafu wa Tanzania Mhe. Benjamin William Mkapa na Jakaya Mrisho Kikwete. Viongozi wengine ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi aliyewakilisha Serikali, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. John Kijazi,   Majaji, Makatibu Wakuu, Mabalozi, wabunge na Viongozi wa Dini.

 

 

 

 

 

Comments (0)

Leave a Comment