Post Details

JAJI MKUU MSTAAFU AUGUSTINO RAMADHANI AMEFARIKI DUNIA LEO JIJINI DAR ES SALAAM

Published By:LYDIA CHURI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salaam za rambirambi kwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma Kufuatia kifo cha Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Augustino Ramadhani aliyefariki dunia leo katika hospitali ya Agha Khan jijini Dar es salaam.

Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani amefariki dunia leo saa 2:05 asubuhi katika Hospitali ya Agha Khan jijini Dar es salaam baada ya kuugua kwa muda mrefu maradhi ya cancer na mwishoni kupata mshtuko wa Moyo (Heart Attack).

Rais Magufuli amempigia simu Jaji Mkuu wa Tanzania na kumpa pole baada ya kupata taarifa ya kifo cha Jaji Mkuu huyo Mstaafu.

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Jaji Mkuu Mstafu Augustino Ramadhani, napenda kutoa pole kwako, familia ya marehemu, waheshimiwa Majaji wote pamoja na watumishi wa Mahakama ya Tanzania”, alisema Rais Magufuli.

Marehemu Jaji Ramadhani alianza kuugua mwaka 2011 na kugundulika kuwa na ugonjwa wa Cancer ambapo alitibiwa katika hospitali mbalimbali nje na ndani ya nchi. Hospitali alizotibiwa ni pamoja na hospitali za Apollo na Bangalow nchini India, Afrika ya Kusini, Nairobi Agha Khan na Dar es salaam Agha Khan.

Marehemu Jaji Augustino Ramadhani alizaliwa tarehe 28/12/1945. Alisoma elimu ya Msingi kati ya mwaka 1952 na 1959 wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma. Mwaka 1960-1965 alisoma kidato cha kwanza mpaka cha sita katika shule ya wavulana ya Tabora (Tabora Boys). Alijiunga na masomo ya Chuo kikuu mwaka 1966 ambapo alisomea fani ya Sheria na kumaliza mwaka 1970.  

Marehemu Jaji Ramadhani alijiunga na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tarehe 26/3/1970 na kulitumikia jeshi hilo mpaka Januari 1978 alipoazimwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu. Wakati wa vita vya Kagera alirejea Jeshini na kwenda vitani mpaka Desemba 1979 aliporejea.

Tarehe 8/1/1980, Marehemu Jaji Augustiono Ramadhani aliapishwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar wadhifa alioushikilia mpaka mwaka 1989 alipoteuliwa na Rais wa awamu ya Pili Mhe. Ali Hassan Mwinyi kuwa 28/6/1989 kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani. Aidha akiwa na wadhifa huo aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Akiwa Mahakamani, aliendelea kupanda vyeo vya kijeshi mpaka kufikia kuwa Brigedia Generali mwaka 1995.  Mwaka 1997 alistaafu kwa hiari Jeshi.

Mwaka 2007, Rais wa awamu ya nne Mhe. Jakaya Kikwete alimteua Jaji Ramadhani kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania ambapo alidumu kwenye cheo hicho mpaka tarehe  27/12/2010 alipostaafu kwa mujibu wa Sheria.

Miongoni mwa nyadhifa nyingine alizowahi kushika ni pamoja na kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu, wadhifa alioushika kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka 2014 hadi mwaka 2016.

Marehemu Jaji Ramadhani pia aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoundwa na Rais wa Awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Julai 4, 2012.

Mipango ya mazishi itajulikana baadaye.

BWANA ALITOA NA BWANA AMETWAA, JINA BWANA LIHIMIDIWE.

 

 

 

 

Comments (0)

Leave a Comment